Trump aiwekea vikwazo ICC kwa kuchunguza jinai za Israel, Marekani
Rais wa Marekani, Donald Trump ametia saini dikrii (amri ya utendaji) ya kuiwekea vikwazo Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) kwa kile alichokiita uchunguzi usio na msingi dhidi ya Marekani na muitifaki wake wa karibu, Israel, kuhusu mauaji ya kimbari huko Gaza.
Agizo hilo la Trump la jana Alhamisi limedai kuwa, mahakama ya The Hague "ilitumia vibaya mamlaka yake" kwa kutoa hati ya kukamatwa Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu, ambaye alifanya mazungumzo na rais huyo wa Marekani siku ya Jumanne.
Amri hiyo pia imedai kuwa, ICC ilijihusisha na "vitendo visivyo halali na visivyo na msingi vinavyolenga Marekani na Israel," ikimaanisha uchunguzi wa ICC juu ya uhalifu wa kivita wa Marekani nchini Afghanistan na mashambulizi ya Israel dhidi ya Gaza.
Agizo hilo linajumuisha kuzuiliwa kwa fedha na marufuku ya kusafiri dhidi ya maafisa wa ICC, wafanyakazi, na jama zao, pamoja na yeyote anayekisiwa kwamba alisaidia uchunguzi wa mahakama hiyo.
Novemba mwaka jana, ICC ilitoa waranti wa kukamatwa Netanyahu na waziri wake wa zamani wa masuala ya vita, Yoav Gallant. Hati hizo ni za "uhalifu dhidi ya ubinadamu na uhalifu wa kivita uliofanywa kuanzia angalau Oktoba 8, 2023 hadi angalau Mei 20, 2024."
Utawala wa Kizayuni na Marekani, ambayo ndiyo muungaji mkono mkuu wa utawala huo, zilishtushwa na kushangazwa na hatua hiyo ya ICC na hivyo zikatoa mijibizo mikali dhidi ya mahakama hiyo.