Waandamanaji New York washinikiza kuachiliwa Mahmoud Khalil
(last modified Fri, 14 Mar 2025 02:30:45 GMT )
Mar 14, 2025 02:30 UTC
  • Waandamanaji New York washinikiza kuachiliwa Mahmoud Khalil

Waandamanaji wanaoiunga mkono Palestina walikusanyika nje ya mahakama ya Manhattan jijini New York nchini Marekani, wakitaka mwanaharakati wa Kipalestina, Mahmoud Khalil aachiliwe huru.

Maandamano ya kupinga kukamatwa kwa Mahmoud Khalil yanaashiria uungaji mkono mkubwa wa haki za Wapalestina na kupinga kufungwa kwa mawakili na wanaharakati wa kisiasa.

Mahmoud Khalil, mhitimu wa Chuo Kikuu cha Columbia aliyekamatwa, ni mwanaharakati mashuhuri wa haki za Wapalestina.

Licha ya kuwa na uhalali wa kuishi Marekani kwa kuwa ana 'kadi ya kijani' ambayo inampa ukazi wa kudumu nchini Marekani, lakini Khalil alikamatwa na kuzuiliwa kwa njia ambayo timu yake ya wanasheria imepinga kuwa ni kinyume cha sheria.

Weledi wa mambo wanasema, mkusanyiko huo wa mawakili wa Kipalestina huko New York kulalamikia kuwekwa kizuizini kwa Mahmoud Khalil, ni ishara ya mshikamano wa kimataifa na watu wa Palestina.

Hii ni katika hali ambayo, Rais wa Marekani Donald Trump amezidisha hatua za ukandamizaji wa wapinzani wa mauaji yanayofanywa na Israel. 

Hivi majuzi alitangaza uamuzi wake wa kuwafukuza Marekani wanafunzi wa kigeni wanaoitetea Palestina na hata kufikia hatua ya kutishia kwamba, wanafunzi wa Marekani wanaoiunga mkono Palestina wanapaswa pia kufukuzwa katika Vyuo Vikuu na kufungwa jela.