UN: Wakati umefika wa kuunda serikali ya shirikishi nchini Syria
Mwakilishi Maalumu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya Syria amesisitiza kuwa, wakati umefika sasa wa kuchukua hatua za dhati na za kijasiri za kuunda serikali ya mpito na ya kuaminika nchini Syria.
Gir Pedersen amesisitiza kuwa: Serikali ya aina hiyo inapasa kuwa ya kweli, yenye kutegemewa na shirikishi ili iwe msingi wa utatuzi wa mgogoro wa Syria.
Pedersen amesema kuwa juhudi zozote za kuasisi serikali ya mpito nchini Syria hazipasi kupelekea kufutwa upande wowote katika mzozo wa nchi hiyo bali makundi yote ya kisiasa yanapaswa kushirikishwa katika serikali hiyo ili kupata njia ya pamoja na ya kudumu kwa ajili ya mustakbali wa Syria.
Mjumbe Maalumu wa UN nchini Syria pia amesisitiza kuwa ipo haja ya kuchukuliwa hatua haraka iwezekanavyo na ametaka kushirikiana pande zote za kikanda na kimataifa li kuunga mkono mchakato huu kwa ajili ya Syria.