Guterres ahudhuria futari ya Waislamu Warohingya wa Myanmar kwenye kambi kubwa zaidi ya wakimbizi duniani
(last modified Sat, 15 Mar 2025 03:05:56 GMT )
Mar 15, 2025 03:05 UTC
  • Guterres ahudhuria futari ya Waislamu Warohingya wa Myanmar kwenye kambi kubwa zaidi ya wakimbizi duniani

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amefuturu na wakimbizi wa Rohingya walioko kwenye kambi kubwa zaidi ya wakimbizi duniani, Cox Baazar nchini Bangladesh kuonyesha mshikamano na wakimbizi hao na wenyeji wanaowapa hifadhi.

Katika futari hiyo iliyofanyika jana Ijumaa, na huku akiwa ameandama na Mshauri Mkuu wa serikali ya Bangadesh Muhammad Yunus, Guterres aliwaambia wakimbizi Waislamu wa jamii ya Rohingya wa nchini Myanmar: “nimefika Cox’s Bazar katika mwezi huu mtukufu wa Ramadhani kwa dhamira ya kuonyesha mshikamano.”

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amepongeza uimara wa Waislamu wa jamii ya Rohingya, walioikimbia nchi yao ya Myanmar baada ya miongo ya mateso na akasisitizia haki yao ya kurudi makwao kwa usalama na hiari, lakini akathibitisha kwamba hali ya usalama nchini mwao Myanmar bado ni mbaya.

Waislamu wanaodhulumika wa jamii ya Rohingya

Akitoa indhari kuhusu upungufu mkubwa wa misaada ya ufadhili, Guterres amesema, “tunakabiliwa na hatari kubwa ya kuwa na asilimia 40 pekee ya rasilimali zilizopatikana mwaka 2024 kwa ajili ya mwaka 2025. Hili litakuwa janga kubwa. Watu wataumia na wengine watapoteza maisha.”

Katibu Mkuu wa UN amesifu pia ukarimu wa Bangladesh katika kuwapa hifadhi wakimbizi hao, lakini akasema changamoto za mabadiliko ya tabianchi, uhaba wa chakula, na kuongezeka kwa hali ya ukosefu wa usalama zinaendelea kuwa kikwazo kikubwa.

Halikadhalika, Guterres amegusia Siku ya Kimataifa ya Kupambana na Uenezaji Chuki Dhidi ya Uislamu (Islamophobia) ambayo huadhimishwa kila tarehe 15 ya mwezi Machi ambayo ni leo Ijumaamosi na akatoa wito kwa jamii ya kimataifa kuonyesha mshikamano na kuongeza misaada ili kuhakikisha wakimbizi Waislamu wa jamii ya Rohingya hawasahauliki. “Katika mwezi huu mtukufu wa Ramadhani, naiomba jamii ya kimataifa ionyeshe mshikamano huo kwa vitendo.” amesisitiza Katibu Mkuu huyo wa UN.../