Hitilafu za viongozi wa Ulaya kuhusu jibu la vita vya ushuru vya Trump
Tangazo la kutoza ushuru mpya la Rais wa Marekani, Donald Trump, dhidi ya nchi 180 duniani, zikiwemo nchi za Umoja wa Ulaya, limeibua hisia tofauti kutoka kwa nchi mbalimbali duniani.
Barani Ulaya, hatua ya Donald Trump ya kutoza ushuru mkubwa wa forodha kwa bidhaa zinazoagizwa nchini Marekani imesababisha hitilafu miongoni mwa viongozi wa Ulaya kuhusu jinsi ya kukabiliana na hatua hiyo iliyoibua mzozo.
Mnamo Aprili 2, 2025 katika "Siku ya Ukombozi" Rais wa Marekani alitangaza ushuru wa "msingi" wa 10% wa kimataifa kwa bidhaa zote zinazoingizwa Marekani. Pia aliweka ushuru wa 25% kwa magari yote ya kigeni yanayoingizwa nchini Marekani.
Kumetokea hitilafu na mgawanyiko wa wazi kati ya nchi wanachama wa EU juu ya suala hili. Wakati Uhispania na Italia zinataka kuepusha mzozo kati yao na Merekani juu ya sera ya ushuru, Ufaransa na Ujerumani zimetaka kutolewe jibu kali zaidi kwa Washington. Waziri wa Uchumi na Biashara wa Uhispania, Carlos Cuerpo amesema: "Tunaendelea kutoa wito wa suluhisho la mazungumzo." Kwa upande wake, Waziri wa Uchumi na Fedha wa Italia, Giancarlo Giorgetti pia amesema: "Lazima tujaribu kudumisha utulivu wetu, kutathmini athari na kuepuka sera ya ushuru wa kulipiza kisasi ambayo ni hatari kwa pande zote, hasa sisi."
Nukta ya kuashiriwa ni kwamba, mapema wiki hii Waziri Mkuu wa Italia, Giorgia Meloni aliutaja ushuru wa Marekani kuwa ni "makosa" na kusema: "Roma itafanya kila iwezalo kufikia makubaliano na Washington ili kuepusha vita vya kibiashara ambavyo vitadhoofisha kambi ya Magharibi dhidi ya wachezaji wengine wa kimataifa."

Haya yanajiri wakati Ujerumani na Ufaransa, chumi kubwa za kwanza na pili katika Umoja wa Ulaya, zimetoa wito wa kutolewa jibu kali zaidi kwa vita vya ushuru wa forodha vya Trump. Ushuru huo utakuwa na athari kubwa kwa Ujerumani, nchi yenye uchumi mkubwa zaidi barani Ulaya, huku mauzo ya Ujerumani kwenda Marekani yakitarajiwa kushuka kwa asilimia 15%. Taasisi ya Kiuchumi ya Ujerumani inakadiria gharama za ushuru huo kwa Ujerumani yenyewe kuwa karibu euro bilioni 200 katika miaka minne ijayo.
Kansela wa Ujerumani, Olaf Scholz ameitaja hatua hiyo kuwa "kimsingi ni kosa" na hujuma dhidi ya utaratibu wa biashara duniani, akionya kuwa sera hizi zitatoa pigo kwa pande zote na kuhatarisha uchumi mzima wa dunia. Waziri wa Uchumi wa Ujerumani, Robert Habeck alisema Aprili 3, siku moja baada ya Trump kutangaza ushuru mkubwa kwa bidhaa za Ulaya kwamba: "Tuko katika nafasi nzuri. Tunaweza kujiunga na nguvu kubwa iliyopo na nchi nyingi na maeneo mengi ya dunia na kuzidisha mashinikizo kwa Wamarekani."
Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron, pia ametoa wito kwa makampuni ya Umoja wa Ulaya kuacha kuwekeza nchini Marekani ili kukabiliana na ushuru wa Trump. "Ni muhimu kwamba uwekezaji wa siku zijazo, uwekezaji uliotangazwa katika wiki chache zilizopita, usitishwe kwa muda hadi tutakapoweka sawa mambo yetu na Merekani," alisema Macron mnamo Aprili 3.
Inaonekana kuwa, athari mbaya za kiuchumi za ushuru mpya wa Trump, ambao unatarajiwa kusababisha mfumuko wa bei na kudumaza ustawi wa uchumi, zimefanya iwe vigumu kwa washirika wa Ulaya wa Washington kukidhi matakwa ya Marekani. Miongoni mwa matakwa hayo ni suala la kuongeza matumizi ya kijeshi ya nchi hizo hadi 3.5% ya Pato la Taifa. Takwa kuu la Rais wa Marekani ni kuongezwa bajeti ya kijeshi ya nchi hizo hadi 5% ya Pato la Taifa.
Tangu Donald Trump alirudi madarakani Januari 20, 2025, uchumi wa dunia na uhusiano wa kibiashara umekabiliwa na changamoto kubwa, na sera zake za kujichukulia maamuzi ya upande mmoja na za utaifa zimeongezeka zaidi. Trump amechochea mvutano na vita vya kibiashara kwa kuweka ushuru mkubwa kwa bidhaa zinazotoka nje ya nchi, ikiwa ni pamoja na ushuru wa 10% kwa bidhaa zote zinazoagizwa kutoka nje na ushuru mkubwa zaidi kwa nchi kama vile China (34%), Umoja wa Ulaya (20%) na Japan (24%). Hatua hizi, mbali na kusababisha tetemeko kubwa katika masoko ya fedha duniani na kudhoofisha thamani ya sarafu ya dola ya Marekani, zimezidisha wasiwasi kuhusu mdororo wa uchumi duniani.

Baadhi ya wachambuzi wameonya kuwa hatua hizi zinaweza kutishia utaratibu wa biashara ya kimataifa. Misimamo na kauli za Trump zinaonyesha nia yake ya kulazimisha matakwa ya Marekani kwa washirika wake wa kibiashara kwa kuweka ushuru mpya na kutishia kuanzisha vita vya kibiashara vya pande zote, jambo ambalo lina maana ya kuvuruga utaratibu wa kiuchumi na kibiashara duniani. Suala hili limeibua wasiwasi mkubwa zaidi katika Umoja wa Ulaya, mojawapo ya washirika muhimu wa kibiashara wa Marekani.
Akizungumzia maamuzi ya Trump, Rais wa Tume ya Ulaya, Ursula von der Leyen amesema: "Kuweka nyongeza ya ushuru dhidi ya dunia nzima ni pigo kubwa kwa uchumi wa dunia na matokeo mabaya makubwa yanaweza kutarajiwa. Mamilioni ya watu watakabiliwa na bili za juu za chakula. Gharama za dawa na usafiri zitaongezeka zaidi. Mfumuko wa bei utaongezeka, na suala hili linawaumiza sana wananchi walio katika mazingira magumu kiuchumi."