Pep Guardiola asikitishwa sana na masaibu ya Wapalestina Gaza
Pep Guardiola, Kocha wa timu ya Manchester City nchini Uingereza, ameelezea kwa uchungu hali ya mateso ya Wapalestina katika Ukanda wa Gaza, akisema ni jambo linalomuumiza sana kila anapofikiria yanayoendelea katika eneo hilo.
Guardiola alitoa kauli hiyo wakati akipokea digrii ya heshima kutoka Chuo Kikuu cha Manchester, kutokana na mchango wake mkubwa ndani na nje ya uwanja kwa jiji hilo. Hafla hiyo ilifanyika katika ukumbi wa kihistoria wa Whitworth Hall, na digrii hiyo ilikabidhiwa na Chansela wa Chuo, Nazir Afzal.
Katika hotuba yake ya kupokea heshima hiyo, Guardiola alisimama kidete kwa ajili ya watu wa Gaza, akilaani kile alichokiita mateso ya wazi yanayoendelea kufanywa na Israel katika vita vinavyoendelea huko Gaza.
Amesema: “Inaumiza mwili wote kuona kinachotokea Gaza”
Wakati akisimama kwa ajili ya Gaza na watu wake, kocha wa Manchester City, Pep Guardiola, ameelezea uchungu wake kuhusu matukio yanayoendelea katika Ukanda wa Gaza kwa zaidi ya mwaka mmoja sasa.
“Ni maumivu makali mno tunayoyaona Gaza. Inaniuma mwili mzima. Na hebu nieleweke vizuri, hili si suala la itikadi... Hapana. Hili ni kuhusu kupenda maisha, kuhusu kujali jirani yako.”
Akizungumzia watoto wake watatu – Maria, Marius na Valentina – Guardiola amesema kwamba kila asubuhi “tangu jinamizi lilipoanza” Gaza, kila anapowaona mabinti zake wawili na mwanawe wa kiume, anakumbuka watoto wa Gaza, jambo ambalo humfanya “kuhisi hofu kubwa sana.”
Takriban nusu ya wakazi wa Gaza, ambao ni jumla ya watu milioni 2.3, ni watoto. Tangu tarehe 7 Oktoba, 2023, Israel imekuwa ikitekeleza mauaji ya kimbardi dhidi ya Wapalestina ambapo imeua watu wasiopungua 55,000 wengi wakiwa ni wanawake na watoto.
Kwa mujibu wa Wizara ya Afya ya Palestina, watoto zaidi ya 17,400 wameuawa, wakiwemo 15,600 waliotambuliwa rasmi. Wengi zaidi bado wamefukiwa chini ya vifusi na wanahofiwa kuwa wamefariki dunia.