Papa Leo aikemea Israel kwa kutumia njaa kama wenzo wa vita
-
Papa Leo wa 14
Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani kwa mara kadhaa sasa tangu achaguliwe kuongoza kanisa Katoliki ameutahadharisha utawala wa Kizayuni wa Israel kuhusu kutumia njaa kama wenzo wa kivita katika Ukanda wa Gaza.
Katika ujumbe aliotuma kwenye kikao cha 44 cha Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO), Papa Leo wa 14 amesema: Katika hali ambayo uzalishaji wa chakula katika baadhi ya sehemu za dunia unazidi mahitaji ya watu, watu wengi duniani bado wanateseka kwa njaa na wataendelea kutaabika kwa ajili ya kukidhi mahitaji yao ya msingi.
Papa ambaye amekuwa akiukosoa utawala wa Kizayuni kwa kutumia njaa kama silaha ya vita, ameongeza kuwa: "Kwa masikitiko na uchungu mkubwa tunashuhudia suala la njaa likitumiwa pakubwa kinyume na ubinadamu kama silaha vitani." Amesema, ni rahisi sana kusababisha njaa kwa jamii za watu.
Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani ameitaka jamii ya kimataifa kuchukua hatua hatua za kuwawajibisha wahusika wa maafa hayo na kuongeza kuwa "Wakati wa vita, wakulima hupoteza uwezo wa kuuza bidhaa zao, bei hupanda kwa kasi na mamilioni ya watu hukabiliwa na njaa na ukosefu wa chakula."
Papa Leo wa 14 pia amesema inasikitisha kuona vyanzo vya fedha na teknolojia ya kisasa vinaelekezwa katika kuzalisha silaha na katika biashara ya zana za kivita badala ya kutumiwa kutatua tatizo la njaa.
Mkutano owa 14 wa Shirika la Chakula na Kilimo Duniani (FAO) ulianza shughuli zake tarehe 28 mwezi Juni huko Roma, mji mkuu wa Italia, na unaendelea hadi tarehe 4 mwezi huu.