Mgombea uongozi wa chama cha UKIP ataka Hijabu ipigwe marufuku Uingereza
(last modified Tue, 09 Aug 2016 06:08:20 GMT )
Aug 09, 2016 06:08 UTC
  • Mgombea uongozi wa chama cha UKIP ataka Hijabu ipigwe marufuku Uingereza

Lisa Duffy, mmoja wa wagombea wa uongozi wa chama cha Uhuru cha Uingereza UKIP ametaka vazi la stara la Kiislamu la Hijabu lipigwe marufuku katika maeneo ya hadhara nchini humo.

Duffy amedai kuwa Hijabu ni nembo ya "kuleta utengano inayoweza kuhamasisha misimamo mikali tu". 

Akihutubia mkutano wa kampeni mjini London, mwanasiasa huyo anayetetea upigaji marufuku vazi la Hijabu nchini Uigereza na ambaye anafananishwa na Donald Trump, mgombea urais wa Marekani kwa tiketi ya chama cha Republican amedai kuwa hatua hiyo itahakikisha kuwepo "usawa" katika jamii na kwamba hatua hiyo eti haitomaanisha chuki dhidi ya Uislamu (Islamophobia).

Mwanasiasa huyo wa chama cha UKIP anataka pia Skuli za Kiislamu zifungwe na kutekelezwa marufuku "kamili na ya pande zote" kwa mahakama za Kiislamu zilizoko nchini Uingereza.

Mwanasiasa Lisa Duffy mwenye kufurutu mipaka na chuki dhidi ya Uislamu

 

Lisa Duffy, ambaye ni mmoja wa wanasiasa sita wa chama cha UKIP wanaowania uongozi wa chama hicho amedai pia kwamba anavyoamini yeye vazi la Hijabu linalazimishwa kwa wanawake na wanaume wanaowaangalia wanawake hao kama milki zao. Mwanasiasa huyo amekwenda mbali zaidi kwa kulifananisha vazi la Hijabu ambalo kulivaa ni faradhi ya kidini yenye utukufu kwa wanawake wa Kiislamu kuwa ni sawa na kuvaa kofia ya helmeti kwenye maeneo ya hadhara.

Duffy mwenye siasa kali za chuki dhidi ya dini ya Uislamu

Chama cha UKIP kitampata kiongozi wake mpya katika mkutano wake wa mwaka utakaofanyika mjini Bournemouth tarehe 15 ya mwezi ujao wa Septemba.

Kiongozi mpya wa chama hicho cha upinzani atarithi nafasi iliyoachwa wazi na Nigel Farage ambaye alijiuzulu baada ya kuongoza kampeni ya kuitoa Uingereza katika Umoja wa Ulaya, hatua iliyochochea mivutano ya uongozi ndani ya chama hicho.../