Je, China imejibu vipi tuhuma za Trump?
https://parstoday.ir/sw/news/world-i130514-je_china_imejibu_vipi_tuhuma_za_trump
Ikiwa ni katika kujibu madai ya Trump, China imetangaza kwamba kupanua ushirikiano wake na nchi nyingine sio tishio kwa nchi yoyote ya tatu.
(last modified 2025-09-07T06:49:34+00:00 )
Sep 07, 2025 06:49 UTC
  • Je, China imejibu vipi tuhuma za Trump?

Ikiwa ni katika kujibu madai ya Trump, China imetangaza kwamba kupanua ushirikiano wake na nchi nyingine sio tishio kwa nchi yoyote ya tatu.

Akizungumza karibuni hivi na waandishi wa habari, Guo Jiakun Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China amejibu kauli ya Rais Donald Trump wa Marekani aliyedai kuwa kuna "njama" kati ya Beijing, Moscow na Pyongyang, kwa kusema: "Kuendelezwa uhusiano wa China na nchi nyingine sio njama wala tishio kwa  nchi yoyote ya tatu." Amesisitiza kuwa: "China kamwe haitalenga nchi ya tatu katika uhusiano wake wa kidiplomasia na mataifa mengine."

Msaidizi wa Rais wa Russia anayehusika na masuala ya sera za kigeni pia amejibu madai ya rais wa Marekani kuhusu mkutano wa viongozi wa China, Russia na Korea Kaskazini mjini Beijing kwamba: "Hakuna mmoja kati ya viongozi hao aliyepanga njama wala hata kufikiria suala hilo akilini."

Rais Xi Jinping wa China, Vladimir Putin wa Russia na Kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong Un, walishiriki katika gwaride kubwa la kijeshi huko Beijing Jumatano iliyopita kuadhimisha miaka 80 ya kumalizika Vita vya Pili vya Dunia.

Kuhusiana na gwaride hilo la kijeshi la kuadhimisha Siku ya Ushindi mjini Beijing, Rais Trump alieleza wasiwasi wake kuhusu ukaribu wa viongozi wa China, Russia na Korea Kaskazini, na kudai kuwa unafuatilia njama dhidi ya Marekani. 

Sherehe za maadhimisho ya miaka 80 ya ushindi katika vita vya mapambano vya watu wa China dhidi ya uvamizi wa Japan na Vita vya Dunia dhidi ya Ufashisti zilifanyika Jumatano katika uwanja wa Tiananmen katikati mwa mji wa Beijing. Hafla hii ilihudhuriwa na viongozi wakuu wa nchi takriban 25 akiwemo Rais Mosoud Pezeshkian wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Ilianza kwa hotuba ya Rais Xi Jinping wa China, ikifuatiwa na gwaride la kijeshi lililowahirikisha maelfu ya wanajeshi, zaidi ya marubani 100 wa ndege za kivita na maonyesho ya mamia ya vitengo vya zana za nchi kavu vya Jeshi la China.

Baadhi ya viongozi waliohudhuria maadhimisho ya Siku ya Ushindi mjini Beijing

Wakati wa kufanyika gwaride hilo, uwezo mbalimbali wa mashambulizi na ulinzi wa jeshi la China ulionyeshwa katika vitengo vya ndege zisizo na rubani, anga, baharini na nchi kavu, ambapo waliohudhuria walishuhudia ndege mbalimbali za kivita zikiruka angani. Katika hafla hii, Beijing ilionyesha kwa mara ya kwanza kombora lake la nyuklia la kimkakati la DF-5S la kati ya mabara. Kombora hilo linalotumia mafuta ya kioevu linaweza kupiga sehemu yoyote ya sayari ya Dunia. Zaidi ya hayo, katika gwaride hilo, China pia imeonyesha kwa mara ya kwanza vikosi vyake vya kimkakati vya nchi kavu, majini na angani zikiwa pande tatu za nyuklia.

Wachambuzi wa mambo ya nchi za Magharibi wamekiri kwamba gwaride kuu la China liliandaliwa kwa uangalifu mkubwa ili kutuma ujumbe wa wazi wa kisiasa kwa Marekani na washirika wake. Katika hotuba yake ya ufunguzi, Rais Xi Jinping alionya kwamba dunia inakabiliwa na "machaguo mawili kati ya amani na vita" na kusisitiza kwamba China haitawahi kuogopa taifa lolote linalotumia mabavu. Gazeti la The Guardian limetafsiri matamshi hayo kama dokezo la wazi kwa Marekani na washirika wake. Xi Jinping pia amekumbusha kwamba watu wa China daima wamekuwa na umoja na kuonyesha mapambano ya kijasiri dhidi ya maadui.

Gazeti la Marekani la New York Times pia limechambua matokeo ya gwaride la kijeshi la Siku ya Ushindi nchini China na kusema kwamba China imeonyesha ulimwengu kuwa kuna njia mbadala ya uongozi wa mabavu wa Marekani duniani. Chini ya anwani "China, Russia, Iran na Korea Kaskazini Zinaelewa vizuri Nafasi Yao", limeeleza kuwa, wakati Xi Jinping anapoandaa maonyesho makubwa ya kijeshi kama hayo huko Beijing, hilo linakuwa zaidi ya kuonyesha tu ndege kadhaa za kivita na makombora. Xi Jinping, ambaye alizungukwa na viongozi wa Russia, Iran na Korea Kaskazini, alikuwa akituma ujumbe wa wazi kwa ulimwengu kwamba kuna njia mbadala inayotegemeka zaidi kuliko uongozi wa Marekani, na kwamba China, kwa kushirikiana na nchi hizo, inaweza kubadilisha mfumo wa mabavu unaotawala sasa ulimwenguni, unaoongozwa na Marekani.

Kwa mujibu wa wachambuzi wa mambo ya nchi za Magharibi, gwaride kuu la China lililofanyika mjini Beijing siku ya Jumatano si tu kwamba lilikuwa onyesho la nguvu za kijeshi, bali pia lilikuwa jukwaa la maonyesho ya ushirikiano wa kisiasa kati ya China, Russia, Iran na Korea Kaskazini, tukio ambalo linapinga waziwazi utawala wa mabavu wa nchi za Magharibi ulimwenguni.