Baada ya machafuko ya umwagaji damu, Nepal yateua Waziri Mkuu wa kwanza mwanamke; UN yakaribisha
Mashirika ya Umoja wa Mataifa yanayohudumu nchini Nepal yamekaribisha kuteuliwa Sushila Karki kuwa Waziri Mkuu wa mpito, wakati nchi hiyo ikikumbwa na mshtuko kufuatia ukandamizaji wa umwagaji damu dhidi ya maandamano yaliyoongozwa na vijana, ambayo yalisababisha vifo vya zaidi ya watu 50, uharibifu mkubwa wa mali na kujiuzulu kwa mtangulizi wake.
Bi. Karki, ambaye ni Waziri Mkuu wa kwanza mwanamke nchini Nepal, aliteuliwa jana Ijumaa na Rais Ram Chandra Poudel, ambaye alimwapisha katika hafla iliyohudhuriwa na wawakilishi wa vijana, maafisa wa serikali na wanadiplomasia wa kigeni.
Kwa mujibu wa vyombo vya habari, waziri mkuu huyo mpya wa mpito amepewa jukumu la kuandaa uchaguzi mpya ndani ya kipindi cha miezi sita.
Kabla ya hapo, Karki aliwahi kuhudumu katika wadhifa wa Jaji Mkuu, akiwa mwanamke wa kwanza kushika nafasi hiyo, na kuongoza Mahakama ya Juu ya Nepal kati ya mwaka 2016 hadi 2017.
Hanna Singer Hamdy, Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa nchini Nepal amesema: “katika kipindi hiki cha mabadiliko muhimu, Umoja wa Mataifa unasimama pamoja na watu wa Nepal katika matarajio yao ya amani, haki, uwazi, uwajibikaji na maendeleo”.
Kupitia taarifa rasmi, Hamdy ametambua mchango wa Rais, Mkuu wa Majeshi na viongozi vijana wa kizazi cha "Gen Z", akibainisha kuwa juhudi zao “zimesaidia kufanikisha kipindi hiki cha mpito.”
Taarifa hiyo imeongeza kuwa Umoja wa Mataifa utaendelea kushirikiana na Serikali ya Nepal ili kuunga mkono utulivu, haki za binadamu na maendeleo endelevu.
Shirika la Watoto la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto, UNICEF limempongeza Bi. Karki, likisema kuwa uteuzi wake “ni motisha kwa wasichana na wanawake,” na likasisitizia umuhimu wa kuweka haki za watoto katikati ya mchakato wa kuijenga upya Nepal.
Mashirika mengine ya Umoja wa Mataifa, ambayo ni la Mpango wa Maendeleo UNDP, Masuala ya Wanawake, UN Women na Afya na Idadi ya watu, UNFPA nayo pia yameeleza kuunga mkono uongozi wake, wakisisitiza juu ya uongozi jumuishi, usawa wa kijinsia, na ulinzi kwa wanawake na vijana.../