Kremlin: Russia haina mpango wa kushiriki mkutano wa 'Bodi ya Amani'
https://parstoday.ir/sw/news/world-i136562-kremlin_russia_haina_mpango_wa_kushiriki_mkutano_wa_'bodi_ya_amani'
Ikulu ya Russia ya Kremlin imethibitisha kwamba maafisa wa nchi hiyo hawana mpango wa kuhudhuria mkutano wa kwanza wa Bodi ya Amani (ya Gaza) uliopangwa kufanyika Februari 19 huko Washington.
(last modified 2026-02-13T05:47:10+00:00 )
Feb 13, 2026 02:03 UTC
  • Dmitry Peskov
    Dmitry Peskov

Ikulu ya Russia ya Kremlin imethibitisha kwamba maafisa wa nchi hiyo hawana mpango wa kuhudhuria mkutano wa kwanza wa Bodi ya Amani (ya Gaza) uliopangwa kufanyika Februari 19 huko Washington.

Msemaji wa Rais Vladimir Putin wa Russia, Dmitry Peskov amesema, "Hakuna yeyote kutoka Kremlin anayepanga chochote." Peskov ameiambia kanali ya Russia ya televisheni ya RTVI kwamba, pendekezo la mkutano huo kwa sasa linapitiwa upya na Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia.

Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya kimataifa vikinukuu barua za mwaliko, vimesema mkutano huo unatarajiwa kuwa kikao cha kwanza cha uongozi wa bodi hiyo na jukwaa la kuchangisha fedha kwa 'ajili ya ujenzi mpya wa Ukanda wa Gaza', chini ya mpango uliozinduliwa na Rais wa Marekani Donald Trump.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia hapo awali iliuelezea mpango mpana wa amani kama "maendeleo chanya" kwa kuzingatia kwake kukomesha umwagaji damu na kutatua masuala ya kibinadamu, ingawa Moscow inasisitiza kwamba juhudi zaidi zinahitajika kushughulikia sababu kuu za ukosefu wa utulivu wa kikanda.

Wakati huo huo, vyombo vya habari vimenukuu ofisi ya Rais wa Belarus, Alexander Lukashenko ikithibitisha kwamba, ingawaje kiongozi huyo amepokea mwaliko wa mkutano huo, lakini hataweza kuuhudhuria.

Kadhalika Italia imesema haiwezi kujiunga na "Bodi ya Amani" ya Rais wa Marekani Donald Trump kutokana na "mpaka wa kikatiba" ukiwa ni mkwamo mpya na wa karibuni zaidi kukikabili "chombo hicho cha kimataifa cha kujenga amani", alichojibunia rais wa Marekani. Itakumbukwa kuwa mwezi uliopita, Trump alizialika karibu nchi 60 kujiunga na bodi hiyo.