Waislamu wa mji wa New York waadhimisha 'Siku ya Waislamu'
Waislamu nchini Marekani wamemiminika katika mitaa ya mji wa Manhattan, New York kuadhimisha 'Siku ya Waislamu' mjini hapo.
Matembezi hayo ya 31 ya kila mwaka ya jamii ya Waislamu nchini Marekani yalianzia katika barabara ya 38 ya Manhattan ambapo washiriki walibeba maua mikononi mwao kama ishara ya upendo.

Kusoma mashairi, na nyimbo zenye jumbe za kidini, kugawa vyakula na vinywaji na kadhalika kutekelezwa shughuli mbalimbali za kifamilia na kirafiki, ni sehemu ya ratiba zilizofanywa kando na maadhimisho hayo ya 'Siku ya Waislamu' mjini hapo.

Matembezi hayo yaliongozwa na Khazer Khan, baba wa Homayoun, askari wa kikosi cha nchi kavu cha jeshi la Marekani ambaye alifariki dunia mwaka 2004 katika mapigano huko nchini Iraq. Aidha maafisa wa polisi Waislamu mjini New York nao walishiriki matembezi hayo ya amani. Inafaa kuashiria kuwa, Waislamu nchini Marekani wameongeza harakati mbalimbali za kuiarifisha dini ya Kiislamu, kutokana na ongezeko la vitendo vya chuki dhidi ya dini hiyo.