Malalamiko ya raia wa Korea Kusini juu ya kuwekwa ngao ya makombora ya Marekani
(last modified Mon, 03 Oct 2016 11:50:28 GMT )
Oct 03, 2016 11:50 UTC
  • Malalamiko ya raia wa Korea Kusini juu ya kuwekwa ngao ya makombora ya Marekani

Wakazi wa mkoa wa Gimcheon, kaskazini mwa Korea Kusini, wamefanya maandamano katika kulalamikia ngao ya makombora aina ya THAAD ya Marekani karibu na mji huo.

Awali ngao hiyo ilikuwa imepangwa kuwekwa katika eneo la Seongju, hata hivyo kutokana na upinzani mkali wa wakazi wa eneo hilo, serikali ya Korea Kusini ililazimika kutangaza kubadili mahala pa kuwekwa ngao hiyo na kwamba sasa itawekwa katika mji wa Gimcheon. Hata hivyo wakazi wa mji huo nao wameanzisha maandamano kupinga kuwekwa mjini humo na wameitaka serikali ya Seoul, kutojaribu kufanya hivyo.

Mandhari ya Ngao ya THAAD ya Marekani kabla ya kusimikwa

Baada ya kutangazwa kufikiwa makubaliano kati ya Marekani na Korea Kusini juu ya kuwekwa ngao hiyo, kulishuhudiwa katika baadhi ya miji ya Korea Kusini maandamano ya wananchi kupinga uamuzi huo. Baada ya makubaliano hayo Seoul na Washington zilitangaza kuwa, hadi kufikia mwishoni mwa mwaka 2017 zitakuwa zimekamilisha uwekaji wa ngao hiyo ya THAAD kwa ajili ya kuzuia kile zilichokitaja kuwa ni tishio la makombora ya Korea Kaskazini.

Rais  Park Geun-hye wa Korea Kusini

Mbali na Korea Kusini, serikali ya Marekani pia ilitangaza kuwa uamuzi wa kuwekwa ngao hiyo nchini Korea Kusini ni kulinda maslahi yake na ya waitifaki wake kutokana na hatari ya Pyongyang. Katika radiamali yake juu ya uamuzi huo, Korea Kaskazini ilitangaza kuibadili ngao hiyo kuwa moja ya shabaha zake za kwanza katika mashambulizi yake huko Korea Kusini. Kwa mtazamo wa Korea Kaskazini, kuwekwa ngao ya makombora ya Marekani aina ya THAAD ndani ya nchi jirani, ni kati ya hatua za kijeshi za White House za kupenda kujitanua katika Peninsula ya Korea.

Sehemu ya majaribio ya makombora ya Korea Kaskazini

Kufanyika maonyesho kadhaa ya kijeshi kati ya Marekani na Korea Kusini katika peninsula hiyo, kunathibitisha madai ya Pyongyang ya kushadidi siasa za kijeshi katika eneo hilo. Mbali na malalamiko ya ndani nchini Korea Kusini, malalamiko kama hayo ya kupinga kuwekwa ngao hiyo ya kijeshi, yameshuhudiwa pia katika nchi za eneo hilo. Uchina na Russia zimepinga vikali mpango wa Marekani na Korea Kusini kuhusiana na suala hilo. Beijing inaamini kuwa, rada za ngao hiyo zinaweza kudukua makombora ya China, suala ambalo linatishia usalama wa taifa hilo. Hata hivyo na licha ya kuendelea upinzani huo, Rais Park Geun-hye wa Korea Kusini amesisitiza kuwa kamwe hatosalimu amri mbele ya matakwa ya wapinzani na wakosoaji wa mpango huo. Rais  Park Geun-hye amesema kuwa, matumizi ya ngao ya makombora ya THAAD ni njia bora ya kulinda usalama wa raia na nchi yake kutokana na vitisho vya Korea Kaskazini. Hata hivyo upinzani wa wananchi juu ya suala hilo, unaashiria kwenda kinyume rais huyo na matakwa ya raia wa nchi yake.

Kiongozi wa Korea Kaskazini

Hii ni kusema kuwa, upinzani juu ya ngao ya makombora ya Marekani aina ya THAAD, hauishii kwa wananchi pekee, bali hata baadhi ya makundi ya kisiasa ya nchi hiyo yameungana na wananchi katika kulalamikia hatua hiyo. Kwa kutumia madai ya kukabiliana na hatari mashambulizi yanayoweza kufanywa na Korea Kaskazini, serikali ya Seoul imeazimia kuweka ngao ya makombora nchini kwake, katika hali ambayo uamuzi huo utashadidisha tu migogoro wa kisiasa na ushindani wa nyuklia katika Peninsula ya Korea.