Unicef yatahadharisha kuhusu kimbunga cha Mathew
Mfuko wa Kuhudumia Watoto wa Umoja wa Mataifa (Unicef) umeripoti kuwa watoto zaidi ya milioni nne nchini Haiti wanakakabiliwa na hatari ya uharibifu iliyosababishwa na kimbunga cha Mathew kilichoathiri visiwa vya eneo la Caribean.
Marc Vincent Mwakilishi wa Shirika la Unicef nchini Haiti ameeleza kuwa hicho ni kimbunga kibaya zaidi kuwahi kushuhudiwa huko Haiti katika miongo ya hivi karibuni na kwamba madhara yake bila shaka yatakuwa makubwa. Mwakilishi wa Unicef nchini Haiti ameongeza kuwa magonjwa yanayosababishwa na kuchafuka maji ni tishio la kwanza litalowakabili watoto katika mazingira ya sasa baada ya kimbunga hicho na kwamba shirika hilo linatoa kipaumbele kwa suala la kuwadhaminia watoto wa nchi hiyo maji ya kutosha.
Katika hali ambayo Haiti ingali ipo katika marhala ya kujijenga upya baada ya kuathiriwa na tetemeko la ardhi mwaka 2010, raia elfu 55 wa nchi hiyo wangali wanaishi katika makazi ya muda huku asilimia 40 ya wengine wakitumia maji yasiyo salama katika maisha yao ya kila siku. Kimbunga cha Mathew ambacho kinakwenda kwa kasi ya karibu kilomita 215 kwa saa tayari kimefika katika pwani ya mashariki mwa Cuba baada ya kusababisha madhara huko Haiti.