Waislamu duniani wakumbuka kuuawa Shahidi Imam Hussein AS
Leo Jumatano inasadifiana na tarehe 10 Mfunguo Nne Muharram, siku ya Ashura ya mapambano ya Imam Husain AS huko Karbala. Maombolezo ya kukumbuka siku hiyo ya majonzi yanawashirikisha Waislamu na hata wasiokuwa Waislamu kote duniani.
Tukio hilo lolojiri siku kama ya leo miaka 1377 iliyopita kulingana na kalenda ya Hijria Qamaria, ambapo moja kati ya vita mashuhuri katika historia ya Kiislamu na ya mwanadamu, vilitokea baina ya majeshi ya haki na batili katika ardhi ya Karbala huko Iraq. Siku hii inajulikana kwa jina la Ashura. Katika siku hiyo mjukuu wa Mtume Muhammad (saw), Imam Hussein bin Ali bin Abi Twalib AS, alisimama kishujaa na wafuasi wake waaminifu 72, kukabiliana na jeshi la batili la Yazid bin Muawiya ili kuilinda dini ya Allah.
Waislamu katika kona zote za Iran wanakusanyika katika kukumbuka siku hiyo kwa kuhudhuria kwa wingi kwenye Husainia, misikiti, haram ya Imam Ridha AS, Imam wa Nane wa Waislamu wa Kishia iliyoko Mash'had, kaskazini mashariki mwa Iran, kama ambavyo pia walikusanyika kwa wingi mno katika Haram ya Bibi Maasuma SA katika mji wa Qum, kusini mwa Tehran na katika maeneo mengine muhimu ya kidini, mitaani na majumbani kwa ajili ya kuomboleza siku hiyo ambayo Imam Husain AS na wafuasi wake wachache, walithibitisha kivitendo kuwa, damu inaweza kuushinda upanga katika medani ya mapambano.
Sisi hapa katika Shirika la Utangazaji la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran IRIB, tunachukua fursa kutuma salamu zetu za rambi rambi kwa Waislamu na hasa wa madhehebu ya Shia ambao wanaikumbuka siku hii ya Ashura kwa majonzi na maombolezo.