Oct 14, 2016 07:44 UTC
  • Russia: Mashambulizi ya Marekani dhidi ya jeshi letu Syria yatajibiwa haraka

Kamanda wa operesheni za jeshi la Russia amesema kuwa shambulizi lolote litakalolenga askari wa nchi hiyo nchini Syria litakuwa na taathira hatari sana.

Sergei Rudskoy ametoa radiamali hiyo baada ya duru za habari kueleza uwezekano wa ndege za kivita za Marekani kushambulia maeneo ya jeshi la Syria. msimamo huo wa Russia umebainishwa baada ya kuenea habari kwamba ikulu ya Marekani (White House) inajadili machaguo ya kijeshi kuhusu mgogoro wa Syria. Inatarajiwa kuwa Rais Barack Obama wa Marekani leo atafanya kikao na washauri wa masuala ya usalama wa taifa kuhusiana na chaguo la kijeshi kwa ajili ya mgogoro wa Syria.

Sergei Rudskoy, Kamanda wa operesheni za jeshi la Russia. 

Inaelezwa kuwa, katika kikao hicho kutajadiliwa suala la kushambuliwa kambi za jeshi, maghala ya silaha na vutuo vya ulinzi wa anga vya jeshi la Syria. Duru za habari nchini Marekani zimearifu kuwa hujuma hizo zitatishia kwa kiwango kikubwa askari wa Russia nchini Syria.

Kwa sababu hiyo Sergei Rudskoy amesisitiza kuwa, kitendo chochote cha chokochoko za Marekani dhidi ya askari wake nchini Syria kitakabiliwa na jibu kali. Afisa huo wa ngazi ya juu wa kijeshi la Russia amesema kuwa, Moscow inaunga mkono mpango wa mjumbe maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya Syria Staffan de Mistura, juu ya kudhaminiwa usalama wa makundi ya wanamgambo wabeba silaha kutoka mashariki mwa mji wa Aleppo.

Rais Vladmir Putin wa Russia 

Hayo yanajiri katika hali ambayo Rais Vladimir Putin wa Russia ametangaza kuwa, Moscow haipo tayari kufanya mazungumzo na Washington. Amesema kuwa, kwa mtazamo wa Marekani neno 'mazungumzo' ni yale yatakayokuwa na maslahi kwa Washington na kuushinikiza upande mwingine. Rais Putin amesema kuwa, nchi yake haipo tayari kufanya mazungumzo ya upande mmoja kuutwisha wa pili matakwa yake.

Tags