Serikali ya Myanmar yazuia misaada kufikishwa kwa Waislamu wa nchi hiyo
https://parstoday.ir/sw/news/world-i17791-serikali_ya_myanmar_yazuia_misaada_kufikishwa_kwa_waislamu_wa_nchi_hiyo
Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) limetangaza kuwa serikali ya Myanmar imezuia misaada ya chakula kufikishwa kwa Waislamu wa Kabila la Rohingya wanaoishi katika jimbo la Rakhine kaskazini magharibi mwa nchi hiyo.
(last modified 2026-02-25T11:30:13+00:00 )
Oct 20, 2016 07:49 UTC
  • Serikali ya Myanmar yazuia misaada kufikishwa kwa Waislamu wa nchi hiyo

Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) limetangaza kuwa serikali ya Myanmar imezuia misaada ya chakula kufikishwa kwa Waislamu wa Kabila la Rohingya wanaoishi katika jimbo la Rakhine kaskazini magharibi mwa nchi hiyo.

Kwa mujibu wa mashuhuda, vikosi vya jeshi la Myanmar vimewekwa katika maeneo ya kaskazini mwa jimbo la Rakhine na karibu na mpaka wa pamoja wa nchi hiyo na Bangladesh na kwamba hawaruhusu kufikishwa misaada ya chakula katika eneo hilo ambalo wakaazi wake waliowengi ni Waislamu.

Kufuatia mauaji yaliyotokea mwanzoni mwa wiki iliyopita ya askari polisi tisa wa Myanmar waliouawa karibu na mpaka wa Bangladesh, serikali ya Myanmar imechukua hatua kali zaidi za usalama katika jimbo la Rakhine na kudai kwamba Waislamu wa kabila la Rihingya ndio waliohusika na mauaji hayo.

Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani limetangaza kuwa kila siku limekuwa likitoa misaada ya chakula kwa watu kati ya elfu 80 hadi 85 katika maeneo yaliyozingirwa na jeshi, lakini katika siku za karibuni jeshi hilo limezuia kufikishwa misaada hiyo ya chakula katika maeneo hayo.

Wanajeshi wa Myanmar wakidhibiti usalama katika maeneo ya Waislamu

Arsin Sahakiyan, mwakilishi wa WFP nchini Myanmar amesema wanajeshi wametawanywa kila mahala na marufuku ya kutotoka nje inatekelezwa hivyo ni jambo lisilowezekana kuyafikia maeneo hayo.

Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa Waislamu wa kabila la Rohingya ni jamii ya wachache duniani inayodhulumiwa na kunyongeshwa zaidi. Serikali ya Myanmar inakataa kuwapa haki za uraia Waislamu ambao idadi yao ni zaidi ya watu milioni moja na laki tatu.

Katika miaka ya karibuni, Waislamu wengi wa kabila la Rohingya nchini Myamnar wameuawa au kulazimika kuhama makazi yao na kuwa wakimbizi katika nchi za Thailand, Malaysia na Indonesia kutokana na mashambulio ya mabudha wenye misimamo ya kufurutu mpaka wanaoungwa mkono na serikali ya nchi hiyo.../