Polisi ya Canada yaahidi kushirikiana zaidi na Waislamu
Jeshi la polisi la mjini Toronto Canada limeteua afisa maalumu wa masuala ya kidini kwa ajili ya kuwasaidia na kuwaunga mkono kimaanawi maafisa wa polisi Waislamu na kuwa kiungo baina ya polisi na Waislamu wa nchi hiyo.
Shirika la Habari la Kimataifa la Qur'ani Tukufu (IQNA) liliripoti jana (Jumamosi) kuwa, afisa huyo ambaye ni mwalimu wa masuala ya utafiti wa Kiislamu, anajulikana kwa jina la Muslih Khan.
Muslih Khan ambaye ni afisa wa kwanza wa polisi wa masuala ya kidini kwa jeshi hilo mjini Toronto amesema kuwa, polisi wa Canada na Waislamu wa nchi hiyo wanapaswa kuwa na mawasiliano ya karibu na kuzidi kuelewana, ili kwa njia hiyo iwe rahisi kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazojitokeza.
Amesema, jeshi la polisi la Canada lina wakati mgumu wa kukabiliana na vitendo vya chuki dhidi ya Waislamu na linahitajia kuwa na mtu madhubuti wa kuwafafanulia misingi ya Uislamu na vile vile kujibu matamshi ya chuki za kidini yanayoenezwa dhidi ya Waislamu.
Kuna jamii nyingi za wachache nchini Canada na jeshi la polisi la nchi hiyo linafanya juhudi za kuwa karibu na watu wote hao, hivyo limeanzisha kampeni maalumu ya kufanikisha mpango wa "Jamii ya Watu Mbalimbali" ikiwa ni pamoja na kuteua wawakilishi wa watu wa kila jamii ndani na jeshi hilo.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, polisi ya Canada iko mbioni kuteua wawakilishi wa mabaniani na makalasinga ndani ya jeshi hilo.