Watu 54 wafa maji baada ya boti yao kuzama Indonesia
Habari kutoka Indonesia zinasema kuwa, watu 54 wamepoteza maisha baada ya boti waliyokuwa wakisafiria kuzama karibu na kisiwa cha Batam.
Habari zaidi zinasema kuwa, boti hiyo ya kasi iliyokuwa imebeba wahamiaji 101 ilikuwa ikitokea Malaysia kabla ya kusombwa na mawimbi ya bahari katika kisiwa hicho kilichoko Indonesia.
Maafisa wa serikali ya Indonesia wamesema miili ya watu 6 walioghariki kwenye ajali hiyo haijapatikana na kwamba tayari wameokoa wahamiaji 41.
Kadhalika watu watatu waliokuwa wanaiongoza boti hiyo wamekamatwa na polisi ya Jakarta kwa tuhuma za kusafirisha wahajiri nchini humo kinyume cha sheria mbali na kubeba abiria kupita kiasi na kusababisha maafa.
Walionusurika wanadai kuwa wamiliki wa boti hiyo waliwatoza nauli na ada zingine za kuwasafirisha na kuwapeleka nchini humo wakitokea Malaysia.
Itakumbukwa kuwa, watu 330 walifariki dunia baada ya feri yao kuzama karibu na kisiwa cha Sulawesi nchini Indonesia mwaka 2009, moja ya ajali mbaya zaidi kuwahi kushuhudiwa nchini humo katika miaka ya hivi karibuni.