Kuendelea kuuliwa Waislamu wa Myanmar na jeshi la nchi hiyo
https://parstoday.ir/sw/news/world-i19675-kuendelea_kuuliwa_waislamu_wa_myanmar_na_jeshi_la_nchi_hiyo
Taasisi ya Taifa ya Arakan Rohingya ARNO (Arakan Rohingya National Organisation) imetangaza kuwa, Waislamu wasiopungua 150 wameuliwa na wanajeshi wa Myanmar katika kipindi cha siku tano zilizopita katika mkoa wa Rakhin wa magharibi mwa nchi hiyo.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Nov 18, 2016 03:05 UTC
  • Kuendelea kuuliwa Waislamu wa Myanmar na jeshi la nchi hiyo

Taasisi ya Taifa ya Arakan Rohingya ARNO (Arakan Rohingya National Organisation) imetangaza kuwa, Waislamu wasiopungua 150 wameuliwa na wanajeshi wa Myanmar katika kipindi cha siku tano zilizopita katika mkoa wa Rakhin wa magharibi mwa nchi hiyo.

Ko Ko Lin, mmoja wa maafisa waandamizi wa taasisi hiyo yenye makao yake mjini London Uingereza amesema kuwa, serikali ya Myanmar inazuia waandishi wa habari na maafisa wa misaada ya kibinadamu wasiingie kwenye mkoa wa Rakhine  kuona kwa karibu jinai zinazofanywa dhidi ya Waislamu wa Rohingya, ili kuficha jinai zinazofanywa na wanajeshi wake dhidi ya Waislamu. Pamoja na kuchuja sana habari, lakini serikali ya Myanmar imelazimika kukiri kuwa jeshi la nchi hiyo limeua Waislamu 70 wa Rohingya katika machafuko ya siku chache zilizopita. 

Waislamu wanaishi katika mazingira magumu sana nchini Myanmar na pamoja na hayo wanatuhumiwa na serikali eti ni magaidi ili kuhalalisha jinai dhidi yao

 

Wimbi jipya la ukatili dhidi ya Waislamu wa Rohingya katika jimbo la Rakhine lilianza tarehe 9 Oktoba mwaka huu kwa madai kuwa watu wenye silaha wameshambulia vituo kadhaa vya mpakani vya jeshi la serikali, na mauaji hayo yanaendelea hadi hivi sasa. Jeshi la serikali ya Myanmar linadai kuwa, Waislamu wa Rohingya wanahusika kwenye mashambulizi hayo na ndio maana limeanzisha msako wa nyumba kwa nyumba katika jimbo lenye Waislamu wengine la Rakhine na hadi hivi sasa makumi ya Waislamu wameshauawa.

Jinai zinazofanywa na jeshi la Myanmar dhidi ya Waislamu limepelekea mamia ya Waislamu hao kukimbilia katika nchi jirani ya Bangladesh. Wimbi kubwa la ukatili dhidi ya Waislamu wa Myanmar limeanza upya katika hali ambayo taasisi za kimataifa hususan Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa zinaendelea kunyamazia kipya jinai hizo ambazo zinafanywa na jeshi la Myanmar kwa kuvamia nyumba za Waislamu na kunajisi wanawake, kuchoma moto nyumba za Waislamu na kuua hata watoto wadogo. Licha ya kuweko mauaji makubwa dhidi ya Waislamu wa Myanmar ambao wanahesabiwa kuwa ndio watu wanaodhulumiwa zaidi duniani, lakini vyombo vya kimataifa vinaishia tu kusema kwa maneno kuwa eti vinasikitishwa na jinai hizo. Kitendo cha serikali ya Myanmar cha kuzuia waandishi wa habari na maafisa wa misaada ya kibinadamu kuingia katika jimbo la Rakhine ni uthibitisho wa wazi wa kutoheshimu nchi hiyo sheria za kimataifa. Kwa kawaida, katika nchi yoyote kunakotokezea machafuko na vita, pande hasimu huruhusu waandishi wa habari na mashirika ya misaada ya kibinadamu kutembelea maeneo yenye vita na migogoro kwa ajili ya kuwasaidia raia wa kawaida. Lakini jeshi la Myanmar limepiga marufuku jambo hilo na linandelea kufanya mauaji dhidi ya Waislamu tangu mwezi uliopita wa Oktoba, na hivi sasa linawatuhumu Waislamu hao kuwa na uhusiano na makundi yenye misimamo mikali ya nje ya nchi hiyo na hivyo kufungua ukurasa mpya wa jinai kubwa zaidi dhidi ya Waislamu kwa kisingizio cha kupambana na ugaidi. Kupitia madai yake hayo mapya, serikali ya Myanmar ina nia ya kueneza chuki zaidi dhidi ya Waislamu na kuvutia uungaji mkono wa nchi nyingine katika ukandamizaji wake wa kuchupa mipaka dhidi ya Waislamu.

Wanajeshi wa serikali ya Myanmar hawaishii tu kufanya mauaji dhidi ya Waislamu, bali wanachoma moto hata nyuma za Waislamu wasio na ulinzi wa nchi hiyo

 

Madai yasiyo na msingi ya serikali ya Myanmar yanatolewa katika hali ambayo Waislamu wa nchi hiyo wamekanusha vikali madai ya kuwa na uhusiano na kundi lolote lile lenye misimamo mikali. Wanachopigania Waislamu hao ni haki yao ya kawaida kabisa kwa kila mtu, ya kuheshimiwa na kupewa haki zao kama raia wengine wa Myanmar. Ni jambo lisilo na chembe ya shaka kwamba, ukatili unaofanywa na jeshi la Myanmar ni ugaidi wa kiserikali, na serikali ya nchi hiyo haiwezi kulificha jambo hilo hata ikiwasingizia Waislamu wa Rohingya kuwa eti wana uhusiano na makundi yenye misimamo mikali ya nje ya Mnyanmar.