Human Rights Watch yamuonya Trump, yaahidi kumfuatilia
(last modified Fri, 18 Nov 2016 15:08:55 GMT )
Nov 18, 2016 15:08 UTC
  • Human Rights Watch yamuonya Trump, yaahidi kumfuatilia

Mkurugenzi mtendaji wa shirika la kimataifa la haki za binadamu la Human Rights Watch amemtahadharisha rais mteule wa Marekani Donald Trump, juu ya utendaji kazi wake baada ya kuingia madarakani.

Kenneth Roth ameyasema hayo Pasris, mji mkuu wa Ufaransa ambako mbali na kuashiria misimamo ya rais huyo mteule aliyoitoa katika kampeni za uchaguzi, amesema kuwa Trump aliahidi kutumia njia ya kuwamiminia maji kwa kuwakosesha pumzi watuhumiwa wa ugaidi endapo njia hiyo itawafanya wakiri tuhuma dhidi yao. Kutokana na matamshi hayo ya Trump, Kenneth Roth amesema kuwa, shirika la Human Rights Watch litafuatilia kwa karibu mienendo yake yote. 

Donald Trump, rais mteule wa Marekani

Indhari ya mkurugenzi mtendaji Human Rights Watch kuhusiana na rais huyo mteule wa Marekani, imetolewa katika hali ambayo asasi na shakhsia mbalimbali wa kisiasa ndani na nje ya Marekani, wamekuwa wakimuonya Donald Trump kutokana na misimamo yake mikali. Hivi karibuni Rais Barack Obama wa Marekani alimuonya Trump akisema kuwa, karibuni hivi ataona ukweli wa mambo juu ya utekelezaji wa ahadi zake tata alizozitoa kwa Wamarekani wakati wa kampeni na kuongeza kuwa, ni vigumu mno kuweza kuzitekeleza ahadi zake hizo.