UN: 30 elfu wamelazimika kuwa wakimbizi Myanmar tangu Oktoba
Umoja wa Mataifa umesema operesheni kali ya kiusalama inayoendelea kushuhudiwa katika jimbo la Rakhine nchini Myanmar imesababisha makumi ya maelfu ya watu kubaki bila makazi tangu mwezi uliopita wa Oktoba.
Msemaji wa Ofisi ya Kuratibu Misaada ya Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa OCHA amesema kuwa, zaidi ya watu 30 elfu wamelazimika kuwa wakimbizi wa ndani tangu Oktoba 9 katika jimbo la Rakhine, baada ya jeshi la nchi hiyo kuanzisha hujuma dhidi ya Waislamu, kwa madai kuwa walihusika na shambulio dhidi ya askari wa mpakani ambapo maafisa 9 wa polisi waliuliwa.
Huku hayo yakiarifiwa, Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa UNICEF umesema kuwa, mwenendo wa wanajeshi kuwashambulia watoto wadogo wa Rohingya kaskazini mwa jimbo la Rakhine ni wa kutisha na kwamba taasisi hiyo ya UN imepokea ripoti za kunajisiwa na kudhalilishwa watoto wadogo katika eneo hilo.
Hii ni katika hali ambayo, jeshi la Myanmar siku chache zilizopita liliua makumi ya Waislamu wa kabila la Rohingya katika wimbi jipya la ukandamizaji unaofanyika nchini humo dhidi ya jamii hiyo ya waliowachache hususan katika jimbo la Rakhine.
Aidha mamia ya nyumba za Waislamu wa eneo hilo zilichomwa moto magharibi mwa nchi hiyo sambamba na kuendelea ukandamizaji dhidi ya wafuasi wa dini hiyo tukufu.
Jimbo la Rakhine lina zaidi ya Waislamu milioni moja na maelfu miongoni mwao wameuawa na malaki ya wengine kulazimishwa kuwa wakimbizi kutokana na mashambulizi yanayoendelea kufanywa na Mabudha wenye misimamo mikali wakisaidiwa na jeshi la nchi hiyo.