Rakhine, machinjio ya Waislamu wa Rohingya, Myanmar
https://parstoday.ir/sw/news/world-i19798-rakhine_machinjio_ya_waislamu_wa_rohingya_myanmar
Jimbo la Rakhine lenye idadi kubwa zaidi ya Waislamu nchini Myanmar limeendelea kushuhudia ukatili na mauaji ya kutisha dhidi ya wafuasi wa dini hiyo.
(last modified 2026-02-22T02:21:18+00:00 )
Nov 20, 2016 02:40 UTC
  • Rakhine, machinjio ya Waislamu wa Rohingya, Myanmar

Jimbo la Rakhine lenye idadi kubwa zaidi ya Waislamu nchini Myanmar limeendelea kushuhudia ukatili na mauaji ya kutisha dhidi ya wafuasi wa dini hiyo.

Ripoti za hivi karibuni zinasema kuwa serikali ya Myanmar imetangaza kuwa makundi ya kigaidi ndiyo sababu ya mauaji yanayoendelea kufanywa dhidi ya Waislamu. 

Taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Uratibu wa Masuala ya Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa inasema kuwa, tarehe 12 na 13 za mwezi huu wa Novemba na sambamba na kuanza wimbi jipya la ukatili na mauaji yanayofanywa na jeshi la nchi hiyo katika jimbo la Rakhine, Waislamu elfu 15 wa kaumu ya Rohingya waliondoka katika makazi na nyumba zao na kupelekwa kusikojulikana. Jeshi la Myanmar na maafisa wa serikali ya nchi hiyo wanadai kuwa, magaidi kutoka Saudi Arabia, Malaysia na Bangladesh wanahusika na machafuko yanayoendelea katika jimbo hilo dhidi ya Waislamu.

Hapana shaka kuwa, ugaidi unatumia vibaya ghasia za kijamii na machafuko ya kisiasa katika eneo lolote lile na katika mazingira kama hayo inawezekana kuituhumu serikali na jeshi la Myanmar kuwa limezembea katika kuwalinda Waislamu wa nchi hiyo. Hata hivyo ukweli ni kwamba, serikali ya Myanmar imeamua kutafuta sababu za uongo na kutupa mpira katika uwanja wa magaidi kuhusiana na ukatili na mauaji ya Waislamu wa Rohingya. Hatua hiyo ya serikali ya Myamnar imechukuliwa ili kuwatetea na kuwasafisha Mabudha wenye misimamo mikali wanaotumiwa kufanya ukatili na kuua Waislamu.

Wabudha wanaoua Waislamu nchini Myanmar

Kwa sasa kuna fikra kwamba, serikali ya Myanmar inatumia kundi la Mabudha wenye misimamo mikali kwa ajili ya kuimarisha nafasi na nguzo zake. Kwa msingi huo imekuwa ikilitumia na kulizatiti kundi hilo kadiri inavyohitajika.

Myanmar iliongozwa na utawala wa kidemokrasia ilipopata uhuru kutoka kwa mkoloni Mwingireza hapo mwaka 1947 hadi mwaka 1962. Hata hivyo mambo yalibadilika baada ya wanajeshi kutwaa madaraka ya nchi hiyo hapo mwaka 1962. Watawala wa kijeshi waliupa utawala wao jina la Baraza la Amani na Ustawi na kuyafungulia njia baadhi ya makundi ya kisiasa na kidini kama kundi la Mabudha wenye misimamo mikali.

Mwaka 2009 wakati Myanmar ilipolazimika kufanya marekebisho ya ndani na kuachiwa huru mpinzani mkubwa wa serikali, Bi Aung San Suu Kyi baada ya kutumikia kifungo cha nyumbani cha miaka 15, Mabudha waliingia katika uwanja wa siasa wa nchi hiyo kama kundi la kifikra na kisiasa. Kwa hakika tangu mwaka 2009 Mabudha wa Myanmar walitambuliwa kuwa washirika wakuu wa serikali eti isiyo ya kijeshi ya nchi hiyo. Katika kipindi hicho cha kuanzia mwaka 2009 kumeshuhudiwa ukatili na mauaji ya kutisha ya Waislamu hususan katika jimbo la Rakhine.

Waislamu wanaendelea kuuawa Myanmar

Katika miaka ya hivi karibuni jeshi la Myanmar limefanya mashambulizi na ukatili mkubwa dhidi ya Waislamu wa nchi hiyo kwa kisingizio cha kuimarisha amani na utulivu. Katika mashambulizi hayo yanayofanywa kwa ushirikiano na Mabudha wenye misimamo mikali idadi kubwa ya Waislamu wameuawa au kujeruhiwa wakiwa ofisini, mashambani na kadhalika, na malaki ya wengine wamelazimika kuwa wakimbizi.

Jumuiya mbalimbali za kutetea haki za binadamu za kimataifa zimekuwa zikipaza sauti kupinga mauaji yanayoendelea kufanywa dhidi ya Waislamu nchini Myanmar japokuwa taasisi zenye mamkala makubwa zaidi kama Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa zinalaumiwa kwa kushindwa kuchukua maamuzi mazito na hatua za kivitendo dhidi ya watawala wa Myanmar wanaofanya ukatili na mauaji nyuma ya mavazi ya Mabudha wenye misimamo mikali.

Watoto Waislamu wanateseka, Myanmar