Wapinzani US: Tutaendeleza maandamano dhidi ya Trump na hatutorudi nyuma
(last modified Sun, 20 Nov 2016 15:54:39 GMT )
Nov 20, 2016 15:54 UTC
  • Donald Trump, Rais mteule wa Marekani
    Donald Trump, Rais mteule wa Marekani

Wanaharakati nchini Marekani wametangaza azma yao ya kuendeleza maandamano ya kumpinga rais mteule wa nchi hiyo Donald Trump wakisisitiza kuwa Trump si chaguo la raia wa Marekani.

Licha ya kupita wiki mbili tangu rais huyo mteule wa Marekani atangazwe mshindi wa urais, lakini raia bado wako mitaani kuendeleza wimbi la maandamano kwa kumiminika katika mabarabara ya miji tofauti ya nchi hiyo kupinga misimamo ya kibaguzi ya Trump wakisema rais huyo mteule hawakumchagua wao. Waandamanaji wameahidi kuendeleza maandamano hayo kupinga misimamo ya timu ya rais huyo iliyo dhidi ya wahajiri, Waislamu na watu wa matabaka ya wachache. Andy Thayer, mmoja wa wanaharakati na waratibu wa maandamano hayo amenukuliwa akisema kama ninavyonukuu: "Tunafikisha sauti yetu ya hasira dhidi ya Trump." Mwisho wa kunukuu.

Maandamano dhidi ya rais mteule wa Marekani

Huku hali ikiwa hivyo ndani ya Marekani, Wamarekani waishio nje ya nchi nao wamefanya maandamano kupinga ushindi wa mfanyabiashara huyo. Karibu watu 1000 wamemiminika mabarabarani mjini Toronto, Canada kumpinga Trump. Maandamano hayo yamefanyika karibu na mnara wa hoteli inayomilikiwa na rais huyo mteule, ambapo kumeripotiwa kujiri vurugu kubwa baina ya waungaji mkono na wapinzani wake. Polisi wa Canada wamelazimika kuingilia kati ili kumaliza vurugu hizo. 

Maandamano dhidi ya rais mteule wa Marekani nchini Canada

Mbali na Canada, balozi za Marekani katika nchi kadhaa za Ulaya, zimeshuhudia maandamano makubwa ya Wamarekani wanaoishi nje ya nchi hiyo wanaompinga Donald Trump na kuionyesha dunia upinzani wao juu ya mfumo mzima wa demokrasia ndani ya Marekani. Ripoti kutoka nchini Marekani zinaonesha kuwa, hadi sasa makumi ya watu wamekwishauawa katika vurugu za kupinga kutangazwa mshindi Donald Trump.