Marekani yaihakikishia Brazil kuhusu kutoiwekea vikwazo
Afisa mmoja wa ngazi za juu wa Brazil amesema kuwa Marekani imeihakikishia nchi yake kwamba haitaiyawekea vikwazo mashirika na benki zake zinazofanya biashara na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Kwa mujibu wa Rodrigo Azeredo, afisa wa ngazi za juu katika Wizara ya Mambo ya Nje ya Brazil aliyekuwa akizungumza hapo jana Jumatano, Wizara ya Fedha ya Marekani imeihakikishia nchi hiyo kwamba benki za Brazil zinaweza kuendelea kufanya biashara na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran bila ya kukabiliwa na tishio la kuwekewa vikwazo. Amesema viongozi wa Washington wamewahakikishia wenzao wa Brasilia kwamba mashirika ya Brazil yanaweze kuendeleza miamala yao ya mauzo ya ndege na zana nyingine bila ya kuwa na wasiwasi wa kuwekewa vikwazo na Marekani.
Afisa huyo wa Brazil amesema kwamba licha ya kuwa vikwazo dhidi ya miamala ya kibiashara ya Iran na nchi nyingine viliondolewa kufuatia kutiwa saini makubaliano ya nyuklia yanayojulikana kwa jina la Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji JCPOA lakini bado benki za nchi hiyo zina wasiwasi mkubwa wa kuwekewa vikwazo na serikali ya Washington. Rodrigo Azeredo amesema kuwa hakikisho hilo la Marekani linaweza kuchangia pakubwa katika kuimarisha biashara kati ya nchi yake na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Mabadilishano ya biashara kati ya nchi mbili hizi mwaka uliopita yalifikia dola biliani moja na milioni 600.