Dec 01, 2016 04:09 UTC
  • WHO: Nusu ya wanaoishi na HIV kote duniani hawajapimwa

Shirika la Afya Duniani WHO limesema karibu nusu ya watu wanaoishi na virusi vya HIV kote duniani hawana habari wala ufahamu kuwa wameambukizwa virusi hivyo hatari vinavyosababisha ugonjwa wa Ukimwi.

Hayo yamesemwa na Margaret Chan, Mkurugenzi Mkuu wa WHO kwa mnasaba wa Siku ya Ukimwi Duniani ambayo inaadhimishwa kote duniani leo Alkhamisi na kuongeza kuwa, kuna haja ya kuongezwa vifaa vya kupimia virusi hivyo hatari majumbani ikizingatiwa kuwa watu wengi wanaogopa kwenda kupimwa katika hospitali, zahanati na vituo vya afya vya umma.

Margaret Chan, Mkuu wa WHO

Mkuu wa WHO amebainisha kuwa, asilimia 40 ya watu wenye virusi vya HIV vinavyosababisha ugonjwa wa Ukimwi, sawa na watu milioni 14 kote duniani, hawajafanyiwa vipimo kutambua hali zao za kiafya.

Kwa mujibu wa takwimu za Shirika la Afya Duniani, kwa kila watu saba wenye virusi vya HIV barani Ulaya, mmoja hana habari kwamba wameambukizwa na kwamba, bara hilo mwaka jana 2015 limeshuhudia ongezeko la maambukizi mapya ya virusi hivyo hatari. Takwimu za WHO zinasema kuwa, bara la Ulaya limeshuhudia maambukizi mapya 153,407  mwaka uliopita wa 2015, ikilanganishwa na 142,000 mwaka juzi 2014, huku baadhi ya duru za habari zikidai kuwa ongezeko hilo limetokana na wimbi la wahajiri wanaoingia barani humo.

Virusi vya HIV husababisha gonjwa la Ukimwi

Ni vyema kuashiria hapa kuwa, Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa UNICEF ulisema katika Kongamano la 21 la Kimataifa la kupambana na maradhi ya UKIMWI mwezi Julai mwaka huu kuwa, virusi vya HIV na ugonjwa hatari wa UKIMWI ungali sababu kuu ya vifo vya vijana barani Afrika na kubainisha kuwa, asilimia 70 ya watu wanaoishi na ugonjwa huo duniani ni vijana kutoka eneo la kusini mwa Jangwa la Sahara barani Afrika.

Haya yanajiri huku hadi leo hakujawa na matibatu kamili ya UKIMWI. Hivi sasa Afrika Kusini imeanza kuifanyia majaribio chanjo ya virusi vya HIV, hatua ambayo Chris Beyrer, mkuu wa Taasisi ya Kimataifa ya Kupambana na virusi vya HIV, amesema kuna matumaini makubwa ya kutibiwa kikamilifu ugonjwa hatari wa Ukimwi, baada ya majaribio ya miongo kadhaa kufeli.

Tags