Waziri Mkuu wa Uingereza aunga mkono makubaliano ya nyuklia Iran
Msemaji wa Theresa May Waziri Mkuu wa Uingereza amesema kuwa Bi May anaunga mkono kikamilifu Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji (JCPOA) na anataka kutekelezwa kikamilifu makubaliano hayo.
Msemaji wa Waziri Mkuu wa Uingereza alisema Jumatano wiki hii kuwa, London inaendelea kuunga mkono makubaliano ya nyuklia yaliyofiikiwa kati ya nchi za kundi la 5+1 na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Kuhusu uwezekano wa kufutwa makubaliano ya nyuklia ya Iran na Donald Trump Rais Mteule wa Marekani, Msemaji wa Waziri Mkuu wa Uingereza ameeleza kuwa, msimamo wa Uingereza kuhusu umuhimu wa makubaliano hayo ya nyuklia uko wazi kikamilifu na kwamba juhudi kubwa za kidiplomasia zimefanyika ili kufikiwa makubaliano hayo. Akiwa katika kampeni zake za uchaguzi wa Rais nchini Marekani, Donald Trump Rais Mteule wa nchi hiyo alitamka kuwa iwapo angeshinda kiti cha urais angefuta makubaliano ya nyuklia, hata hivyo baada ya kushinda uchaguzi huo, Trump amelegeza msimamo wake huo wa awali.