HRW: Jeshi la Myanmar limeteketeza vijiji vya Waislamu Warohingya
Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch linasema kuna ushahidi unaoonyesha kuwa Jeshi la Myanmar limeteketeza vijiji vya Waislamu wa kabila la Rohingya katika jimbo la Rakhine.
Katika taarifa, HRW inasema ina picha za satalaiti pamoja na mahojiano na mashuhuda kuhusu namna majengo 1,500 yalivyobomlewa katika jimbo lenye Waislamu wengi la Rakhine tokea Oktoba 2015
Mkurugenzi wa Bara la Asia katika Human Rights Watch Brad Adams anasema picha hizo za satalaiti zinabatilisha madai ya serikali na jeshi la Myanmar kuwa wanamgambo ndio walioteketeza nyumba za Waislamu.
Taarifa hiyo imesema idadi ya nyumba za Waislamu zilizoteketezwa moto yamkini ikawa kubwa zaidi kutokana na kuwa eneo hilo limefunikwa na misitu.
Wiki iliyopita Umoja wa Mataifa ulitoa wito kwa kiongozi asiye rasmi wa Myanmar Aung San Suu Kyi achukue hatua za kuzuia ukatili wa jeshi la nchi hiyo dhidi ya Waislamu wa kabila la Rohingya katika jimbo la Rakhine kaskazini mwa nchi hiyo.
Wakati huo huo Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu OIC imepanga kuitisha kikao cha dharura kujadili hali ya Waislamu wa Myanmar. Katibu Mkuu wa OIC Ahmed Al-Othaimeen aidha amelaani ukandamizwaji wa Waislamu wa Myanmar.
Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa Waislamu wa kabila la Rohingya ni jamii ya wachache duniani inayodhulumiwa na kunyongeshwa zaidi. Serikali ya Myanmar inakataa kuwapa haki za uraia Waislamu hao ambao idadi yao ni zaidi ya watu milioni moja na laki tatu.
Katika miaka ya karibuni, Waislamu wengi wa kabila la Rohingya nchini Myamnar wameuawa au kulazimika kuhama makazi yao na kuwa wakimbizi katika nchi za Thailand, Malaysia na Indonesia kutokana na mashambulio ya Mabudha wenye misimamo ya kufurutu mpaka wanaoungwa mkono na serikali ya nchi hiyo