Serikali ya Marekani yawafukuza wanadiplomasia wa Russia
https://parstoday.ir/sw/news/world-i22384-serikali_ya_marekani_yawafukuza_wanadiplomasia_wa_russia
Serikali ya Marekani imewafukuza nchini humo wanadiplomasia wa Russia kitendo ambacho kimeufanya uhusiano wa nchi mbili hizo kuingia katika hatua nyingine.
(last modified 2026-03-03T12:46:59+00:00 )
Dec 30, 2016 00:17 UTC
  • Serikali ya Marekani yawafukuza wanadiplomasia wa Russia

Serikali ya Marekani imewafukuza nchini humo wanadiplomasia wa Russia kitendo ambacho kimeufanya uhusiano wa nchi mbili hizo kuingia katika hatua nyingine.

Taarifa zaidi zinasema kuwa, katika hatua ambayo haikutarajiwa, serikali ya Marekani imetangaza kuwatimua nchini humo wanadiplomasia 35 wa Russia kutokana na kile kilichoelezwa kwamba, hatua ya Moscow ya kuingilia uchaguzi wa Rais wa Marekani wa Novemba mwaka huu.

Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Marekani imewapa wanadiplomasia hao na familia zao muda wa masaa 72 wawe wameondoka katika ardhi ya Marekani.

Mivutano kati ya Marekani na Russia imeshadidi katika siku za hivi karibuni

Taarifa hiyo imesema, wanadiplomasia wa Russia na familia zao walioko mjini Washington na wa ubalozi mdogo mjini San Francisco wamepatiwa muhula wa masaa 72 wawe wameondoka nchini humo na kurejea kwao. Amri hiyo ya kutimuliwa wanadiplomasia wa Russia iliyotolewa na Rais Barack Obama inahesabiwa kuwa ni hatua ya kuiadhibu Moscow kutokana na kuweko taarifa kwamba, ilifanya udukuzi katika uchaguzi wa Rais wa Marekani. Aidha Rais Obama ametoa amri ya kuwekewa vikwazo maafisa 6 wa Russia pamoja na asasi 5 za nchi hiyo.

Rais Obama amekuwa akiituhumu Russia kwamba, ilifanya udukuzi katika uchaguzi wa Rais wa Marekani na kumsaidia Donald Trump kuibuka na ushindi dhidi ya Hillary Clinton. Hata hivyo Russia imekuwa ikikanusha vikali tuhuma hizo na kusema hazina msingi wowote. Kutimuliwa wanadiplomasia hao wa Russia bila shaka kutashadidisha mivutano iliyopo kati ya Moscow na Washington na kuvuruga uhusiano wa kidiplomasia kati ya pande mbili.