Jan 08, 2017 03:10 UTC
  • Ufidhuli wa Israel na Marekani dhidi ya Umoja wa Mataifa

Utawala ghasibu wa Israel umepunguza mchango wake wa kifedha kwa Umoja wa Mataifa kwa kiwango cha dola milioni sita baada ya Baraza la Usalama la umoja huo kupasisha azimio linalopinga ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni unaofanywa na utawala huo katika ardhi za Palestina.

Ujumbe wa Israel katika Umoja wa Mataifa umetangaza kuwa, kiwango hicho cha asilimia 40 ya mchango wa kila mwaka wa Israel kwa Umoja wa Mataifa kimepunguzwa katika sehemu ya bajeti ya umoja huo katika kamati nne zinazohusiana na kadhia ya Palestina. 

Danny Danon, balozi wa utawala wa Kizayuni wa Israel katika Umoja wa Mataifa amedai kuwa, hakuna maana yoyote kwa Israel kuzisaidia taasisi za umoja huo ambazo zinachukua hatua zilizo dhidi ya utawala huo.

Hatua hiyo ya utawala wa Kizayuni dhidi ya Umoja wa Mataifa imechukuliwa katika hali ambayo, utawala huo ghasibu si utawala halali katika uga wa kimataifa na umepata uanachama katika Umoja wa Mataifa kwa mapatano ya kisiasa na sasa unatumia propaganda za kisiasa kuimarisha nafasi yake. 

 

Danny Danon, balozi wa Israel UN 

Baada ya miaka kadhaa ya kuwa kimya na kutochukua hatua, Umoja wa Mataifa hatimaye umelazimika kuitikia wito wa nchi mbalimbali kwa kulaani jinai za utawala wa Kizayuni dhidi ya Wapalestina. Hata hivyo hatua hiyo ndogo imewakasirisha sana viongozi wa utawala wa Kizayuni na waungaji mkono wake. Kitu kinchoautia wasiwasi zaidi utawala wa Kizayuni wa Israel na waungaji mkono wake ni zingatio la Umoja wa Mataifa kwa haki za Wapalestina kimataifa. Katika mazingira hayo, utawala wa Kizayuni na muungaji mkono wake mkuu yaani Marekani, wanafanya kila linalowezekana kueneza propaganda na kutumia mashinikizo ya kifedha ili kubadili mchakato huu na wakati huo huo kuufanya Umoja wa Mataifa kuwa taasisi ya kutumikia malengo ya utawala huo.

Katika fremu hiyo, maseneta wa chama cha Republican katika Congresi ya Marekani ambao pia wamekasirishwa na hatua ya Umoja wa Mataifa ya kupasisha azimio nambari 2334 linalolaani ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni huko Palestina, kwa sasa wanachunguza suala la kusimamisha mchango wa serikali ya Washington katika umoja huo. Marekani ambayo huko nyuma ilikuwa ikiyapigia kura ya turufu maazimio yote yanayotolewa dhidi ya Israel, mara hii ilijizuia kulipigia kura azimio hilo ambalo lilipasishwa kwa kura 14 za ndio kutokana na mashinikizo ya fikra wa waliowengi. 

Maseneta wa chama cha Republican katika Kongresi ya Marekani 

Ni vyema kuashiria hapa kuwa, Marekani inadhamini karibu robo au asilimia 22 ya bajeti ya Umoja wa Mataifa. Nukta muhimu ni kwamba, Marekani licha ya kudhamini sehemu hiyo ya bajeti daima imekuwa ikiingilia masuala mbalimbali duniani na kuusababishia matatizo Umoja wa Mataifa. Marekani imekuwa ikitoa mchango huo wa kimaonyesho ili kuficha jinai zake katika uga wa kimataifa na uungaji mkono wake kwa utawala ghasibu wa Israel. Hasa ikizingatiwa kuwa Marekani imekuwa ikitumia mbinu mbalimbali kupitia misaada hiyo ili kuathiri maamuzi ya Umoja wa Mataifa na kuifanya taasisi hiyo ya kimataifa kuwa wenzo wa kutimizia malengo yake haramu. 

Mwenendo huo wa Marekani na utumiaji wake usiofaa wa kura ya turufu umeufanya Umoja wa Mataifa kuwa kama milki suala ambalo linakwamisha pakubwa juhudi za kutimzia malengo muhimu na makuu ya Umoja wa Mataifa. Hatua hizo za Marekani katika Umoja wa Mataifa zimeutia kiburi utawala wa Kizayuni wa Israel kiasi kwamba taasisi hiyo ya kimataifa imekuwa ikilengwa lwa vitisho kutoka utawala huo.

Ni muda sasa ambapo fikra za waliowengi zinataka kuondolewa utawala haramu wa Israel katika Umoja wa Mataifa na pia kukomeshwa vitisho hivyo vya Marekani. Vilevile jamii ya kimataifa inataka kufanyike marekebisho katika muundo wa Umoja wa Mataifa ili chombo hicho kisidhibitiwe na madola makubwa duniani.   

 

Tags