Apr 18, 2024 10:40 UTC
  • Wawakilishi wa Kongresi: Israel inakiuka sheria kwa kutumia silaha za Marekani kufanya mauaji

Kundi la wawakilishi wa chama cha Demokratic katika Kongress ya Marekani limesisitiza kuwa, utawala wa Israel unakiuka sheria kwa kutumia silaha za Marekani kufanya mauaji na mashambulizi makali huko Palestina.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Iran (IRNA), 

barua iliyoandikwa na wabunge 26 wa Kongresi ya Marekani kwa Waziri wa Ulinzi, Lloyd   Austin, Waziri wa Mambo ya Nje Anthony Blinken na Mkurugenzi wa Ujasusi wa Kitaifa Avril Haines inasema, kinyume na madai ya Rais wa Marekani Joe Biden, jinsi jeshi la utawala wa Kizayuni linavyotumia silaha za Marekani kunapingana na sheria za nchi hii na sheria za kimataifa.

Barua ya wabunge hao wa Marekani inasema, wawakilishi wa Kongresi, taasisi za kiserikali, mahakama za kimataifa na waangalizi wa haki za binadamu wa utawala wa Israel, pamoja na maafisa wa serikali ya Marekani, wamekuwa wakieleza wasiwasi wao mkubwa kuhusu hatua ya Benjamin Netanyahu tangu miezi michache iliyopita.

Kabla ya hapo pia wabunge 40 wa chama cha Democratic katika Bunge la Marekani walimtaka Rais Joe Biden kuacha kuuuzia silaha utawala haramu wa Israel.

Katika barua hiyo, wawakilishi wa Kongresi akiwemo Nancy Pelosi, Spika wa zamani wa Baraza la Wawakilishi, walimtaka Biden kusimamisha uuzaji wa silaha kwa utawala wa Kizayuni na kuweka masharti kwa msaada wa Washington kwa utawala huo.

Kutiwa saini barua hii na wawakilishi wa chama cha Democratic katika Kongresi ya Marekani hususan Nancy Pelosi kunaonyesha jinsi nafasi ya Israel ilivyoporomoka mbele ya wananchi wa Marekani na Chama cha Demokratic kutokana na vitendo vya kikatili, mauaji na jinai zinazofanywa na jeshi la utawala huo katika Ukanda wa Gaza unaokaliwa kwa mabavu.

Bernie Sanders, seneta wa kujitegemea wa Marekani, pia alimtishia Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, na kusema kwamba, ikiwa maelfu ya malori yenye misaada ya kibinadamu hayataruhusiwa kuingia Ukanda wa Gaza unaokaliwa kwa mabavu, misaada yote ya kijeshi ya Marekani kwa utawala huo itasitishwa. 

Corey Bush, mwakilishi wa Kidemokrati wa Bunge la Marekani, pia amesisitiza kuwa Washington inaweza kuwa na taathira katika kusimamisha vita huko Gaza, na ametoa wito wa kusitishwa mapigano mara moja na kwa njia ya kudumu katika eneo hilo.

Tags