Russia: Tutatoa msaada wa kijeshi kwa Cameroon kukabiliana na Boko Haram
Serikali ya Russia imesisitizia udharura wa kuungwa mkono kijeshi juhudi za serikali ya Cameroon kwa ajili ya kupambana na wanachama wa kundi la kigaidi na kitakfiri la Boko Haram nchini humo.
Balozi wa Russia nchini Cameroona, Nikolay Ratsiborinsky amesema kuwa Moscow itatoa zana za kijeshi za kizazi kipya na za kisasa ukiwemo mfumo wa anga, silaha na zana za usafirishaji kwa jeshi la Cameroon ambazo zitatumika katika mapambano dhidi ya genge la kigaidi la Boko Haram.
Wakati huo huo kamisheni ya Umoja wa Afrika imetangaza utayarifu wake wa kutoa silaha, zana za kijeshi na misaada mbalimbali ya kimataifa kwa majeshi ya mataifa kadhaa katika kukabiliana na wanachama wa kundi hilo maarufu kwa kutenda jinai dhidi ya binaadamu. Kundi la Boko Haram ambalo hivi sasa limegeuka na kuwa tishio kubwa kwa usalama na amani ya nchi za eneo la magharibi mwa Afrika, lilianzisha hujuma zake nchini Nigeria hapo mwaka 2009 na kupanua wigo wa mashambulizi hayo nje ya nchi hiyo hapo mwaka 2015.
Hadi sasa mashambulizi ya genge hilo yamepelekea zaidi ya watu elfu 17 kuuawa na mamilioni ya wengine kuwa wakimbizi.