Jan 30, 2017 07:38 UTC
  • 5 wauawa kwa risasi kwenye hujuma dhidi ya msikiti Quebec, Canada

Kwa akali watu watano wameuawa katika hujuma ya kikatili dhidi ya msikiti mmoja katika mji wa Quebec nchini Canada usiku wa kuamkia leo.

Mohamed Yangui, Rais wa Kituo cha Kiutamaduni cha Kiislamu mjini Quebec amesema waumini watano wa Kiislamu waliuawa walipokuwa wakisali Sala ya Ishaa jana usiku, baada ya wavamizi kuvamia msikiti huo na kuwamiminia risasi ovyo. Ameongeza kuwa, watu kadhaa wana majeraha ya risasi kufutia hujuma hiyo ya kinyama.

Polisi katika eneo hilo inadai kuwa imewakamata washukiwa wawili wa hujuma hiyo na kwamba yumkini mmoja amefanikiwa kutoroka.

Nje ya msikiti mjini Quebec, Canada

Waziri Mkuu wa Canada Justin Trudeau amelaani shambulizi hilo dhidi ya msikiti na kulitaja kama hujuma ya kigaidi dhidi ya Waislamu. Katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter, Trudeau amesema: "Tunalaani hujuma hiyo dhidi ya pahala pa kutekelezea ibada na kimbilio la waumini, kitendo hiki ni cha kioga na serikali inatoa mkono wa pole kwa wahanga wa hujuma hii, na tuko tayari kutoa msaada wa aina yoyote kwa familia za wahanga hawa."

Kituo cha Kiutamaduni cha Kiislamu mjini Quebec kimekuwa kikilengwa na watu wenye misimamo ya chuki dhidi ya Uislamu mara kwa mara. Mwezi Juni mwaka jana wakati wa Ramadhani, watu wenye chuki dhidi ya Uislamu na Waislamu waliacha kichwa cha nguruwe katika mlango wa msikiti huo.

Aidha mwaka 2015, msikiti mmoja katika jimbo la Ontario nchini Canada uliteketezwa moto na watu wenye misimamo ya kurufutu ada wanaouchukia Uislamu.

 

Tags