Feb 10, 2017 07:58 UTC
  • Wasiwasi wa kuenea fikra za Uwahabi wa Saudia barani Ulaya

Serikali ya Ubelgiji imeonyesha wasi wasi wake juu ya kuenea mafundisho ya Uwahabi unaoungwa mkono na utawala wa Saudi Arabia ndani ya nchi hiyo na mataifa mengine ya Ulaya.

Ripoti iliyotolewa na Idara ya Usalama nchini Ubelgiji (OCAM) imesema kuwa, vituo Kiislamu vinavyoungwa mkono na Saudia huko barani Ulaya, vinaeneza mafundisho hatari ya Uwahabi. OCAM imeongeza kwa kusema: "Uwahabi ni idiolojia ya misimamo ya kufurutu ada ambayo inaungwa mkono na utawala wa Saudi Arabia ambapo wahubiri wa nchi hiyo wanaeneza kwa uhuru mafundisho hayo kupitia himaya kamili ya Riyadh, huku magaidi duniani kote wakitekeleza jinai zao kwa kutumia idiolojia hiyo.

Sheikh Mkuu wa Kiwahabi nchini Saudia ambaye ni maarufu kwa ukufurishaji wa Waislamu

Daesh na makundi mengine ya kigaidi kwa kutumia idiolojia hiyo ya Uwahabi, yanawakufurisha wafuasi wa madhehebu nyingine za Kiislamu na kuhalalisha mauaji dhidi yao. Tunawatahadharisha maimamu wa sala za jamaa katika misikiti mbalimbali kutokana na kuathirika taratibu na mafundisho hayo ya Usalafi." Mwisho wa kunukuu. Kwa mujibu wa nyraka za siri za WikiLeaks, Hillary Clinton, Waziri wa zamani wa Mambo ya Nje wa Marekani ambaye nchi yake ni mmoja wa waungaji mkono wakubwa wa utawala wa Aal-Saud, alikiri waziwazi kwamba Saudi Arabia ni muungaji mkono mkuu wa kifedha wa makundi ya kigaidi kote duniani, ukweli ambao hii leo umethibitishwa na Idara ya Usalama ya Ubelgiji. Itafahamika kuwa, Ubelgiji ni moja ya nchi za Ulaya ambayo kwa muda mrefu imekuwa ikikabiliwa na harakati za makundi yenye misimamo mikali ya kigaidi.

Baadhi ya masheikh wa Uwahabi akiwahadaa vijana

Hivi sasa nchi hiyo imejiweka katika hali ya tahadhari hasa kufuatia mashambulizi ya kigaidi ya hivi karibuni katika uwanja wa ndege wa mjini Brussels na treni ya chini ya ardhi nchini humo ambapo kwa akali watu 32 waliuawa. Kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh (ISIS) ambalo linapata himaya kamili kutoka Saudia, lilitangaza kuhusika kwake na hujuma hiyo. Kadhalika kundi hilo lilitangaza kuhusika na hujuma nyingine za kigaidi zilizotokea katika miji mbalimbali ya Ulaya kama vile Paris, Ufaransa na Berlin, Ujerumani ambapo makumi ya watu waliuawa na wengine wengi kujeruhiwa. Katika upande mwingine ni kwamba, baada ya kudhihiri kundi la kigaidi la Daesh huko nchini Iraq na Syria, raia wengi wa nchi za Ulaya walielekea katika nchi hizo kwa ajili ya kujiunga na magenge hayo ya kigaidi ambayo yanatokana na fikra za Kiwahabi, ambapo hivi sasa athari mbaya za mgogoro huo zimezidi kupanuka. Hii ni kusema kuwa, asilimia kubwa ya raia wa mataifa hayo ya Ulaya wanaendelea kurejea makwao kutokana na kushindwa mtawalia makundi ya kigaidi katika vita na majeshi ya serikali za Iraq na Syria, ambapo kurejea kwao huko kumeyatia hatarini mataifa hayo.

Viongozi wa kidini na kisiasa wa Saudia ambao wanasaidiana kueneza Uwahabi duniani

Suala hilo ndilo limewazidishia wasi wasi mkubwa viongozi wa kisiasa na kiusalama wa nchi za Ulaya. Hii ni katika hali ambayo katika kipindi cha kuibuka machafuko huko Iraq na Syria, ni madola hayo hayo ya Ulaya ndiyo yaliyojitokeza na kuyaunga mkono kikamilifu makundi hayo ya kigaidi kwa lengo la kuziondoa madarakani serikali halali za nchi hizo. Hata Rais Bashar al-Assad wa Syria kwa mara kadhaa aliyaonya madola hayo ya Ulaya juu ya hatua yao hiyo ya uungaji mkono kwa makundi hayo hatari kwa kuyaambia kwamba mwenendo huo ulikuwa unakinzana na maslahi ya mataifa hayo. Ukweli ni kwamba, hatua ya viongozi na taasisi za usalama barani Ulaya ya kuonyesha wasi wasi wa kuenea mafundisho ya Uwahabi na mashambulizi ya kigaidi, inajiri katika hali ambayo ni nchi hizo hizo kwa kushirikiana na Saudia, ndizo zilihusika katika kuyalea makundi hayo hatari lengo kuu likiwa ni kuibua machafuko na mgogoro ndani ya Iraq na Syria, na hii leo athari mbaya ya magenge hayo sasa imezigeukia nchi hizo hizo za Ulaya.

Vijana wa nchi za Kiislamu ambao tayari wameathirika na ghilba za Uwahabi

Hii leo mubalighina wa Kiwahabi sambamba na kwenda kinyume na mafundisho ya dini ya Kiislamu na kwa kuitumia vibaya dini tukufu ya Kiislamu, wanawahadaa vijana wengi wa nchi za Magharibi kwa ajili ya kujiunga na makundi ya kigaidi yenye kufuata mafundisho ya Kiwahabi. Katika mazingira kama hayo tunaweza kusema kuwa, hivi sasa viongozi wa nchi za Ulaya wanahitaji kuelewa kwamba haipasi kuvihusisha vitendo vya kigaidi na dini ya Uislamu kama ambavyo pia hawatakiwi kueneza chuki dhidi ya dini hiyo hasa kwa kuzingatia kuwa, magaidi hawana dini. Kwa upande mwingine ni kwamba, usalama wa Ulaya utapatikana pale tu nchi za bara hilo zitakapoacha kuunga mkono makundi hayo ya kigaidi maarufu kwa kutenda jinai dhidi ya binaadamu.

Tags