Bunge la Ufaransa lamtaka Rais Francois Hollande kuitambua rasmi Palestina
Wabunge wa Ufaransa wamemtaka Rais wa nchi hiyo Francois Hollande aitambue rasmi Palestina.
Wabunge 153 na wawakilishi wa Baraza la Seneti la Ufaransa wamemuandikia barua Rais wa nchi hiyo Francois Holland na kumtaka aitambue rasmi nchi ya Palestina.
Katika barua hiyo, Wabunge hao wamemtaka Rais Hollande asipoteze fursa hiyo ya kihistoria na badala yake athibitishe ustahiki wake kwa kuitambua rasmi nchi ya Palestina.
Mwaka 2014 Bunge la Ufaransa lilianza kujadili hoja ya kuitambua rasmi nchi ya Palestina. Hoja hiyo iliyowasilishwa na chama tawala cha Kisoshalisti inaungwa mkono na idadi kubwa ya wabunge.
Zaidi ya nchi 135 zimeitambua rasmi nchi ya Palestina huku Sweden ikiwa nchi ya hivi karibuni barani Ulaya kufuata mkondo huo. Nchi zingine za Ulaya zilizotambua rasmi nchi ya Palestina ni pamoja na Uingereza na Uhispania.
Hivi karibuni gazeti la Kizayuni la Yedioth Ahronoth liliandika kuwa, pamoja na kuwa Marekani inaendelea kuunga mkono kikamilifu utawala wa Kizayuni wa Israel, lakini balozi za Palestina zinaendelea kuongezeka duniani na hata kuzishinda zile za Israel.
Gazeti hilo liliandika kuwa, hivi sasa kuna ofisi 103 za uwakilishi wa kidiplomasia huko Palestina ikilinganishwa na 102 zilizoko Tel Aviv. Aidha gazeti hilo limeandika kuwa katika hali ambayo Palestina ina ofisi 95 za uwakilishi wa kidiplomasia katika maeneo mbali mbali duniani, utawala wa Israel una ofisi 78 pekee za uwakilishi duniani.