Sheria mpya ya Trump dhidi ya Waislamu yalaaniwa kote duniani
Sheria mpya ya kibaguzi ya Donald Trump, Rais wa Marekani, inakabiliwa na wimbi la lalama na ukosoaji kutoka kila upande, ndani na nje ya nchi.
Asasi za kutetea haki za binadamu na mashirika ya kidini yamekosoa vikali sheria hiyo na kuitaja kuwa ya kibaguzi na inayokiuka katiba.
Omar Jadwat, Mkurugenzi wa asasi ya kiraia inayofahamika kama The American Civil Liberties Union amesema agizo hili jipya la Trump, kama lile la awali, lina mapungufu mengi ya kisheria na kwamba tayari kuna kesi zaidi ya 12 mahakamani kupinga utekelezwaji wake.
Latika sheria hii mpya Trump imeiondoa Iraq, katika orodha ya nchi saba za Kiislamu ambazo raia na wakimbizi wake hawataruhusiwa kuingia nchini Marekani katika muda wa siku 90 zijazo. Nchi zilizoathiriwa na sheria hiyo ya kibaguzi ya Trump ni Sudan, Somalia, Syria, Iran, Libya na Yemen.
Mashirika mengine ya kutetea haki za binadamu yaliyotoa taarifa za kukosoa vikali sheria hiyo ya Trump ni pamoja na Human Rights Watch, Interfaith Alliance, United Farm Workers of America na The New York Immigration Coalition. Rabbi Jack Moline, Mkurugenzi Mkuu wa muungano wa kidini Marekani wa Interfaith Alliance, amesema sheria hiyo mpya ya Trump haina jipya na kwamba bado ni ya kibaguzi. Amesema: "Lazima tuwekane sawa hapa, kuwabagua watu kwa misingi ya dini na imani zao za kiroho hakuwezi kuifanya Marekani kuwa pahala salama zaidi."
Awali, Zeid Ra’ad Zeid al-Hussein, Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa alitangaza kuwa, amri iliyotiwa saini na Rais Donald Trump wa Marekani ya kuzuia raia wa nchi sita za Kiislamu kuingia nchini Marekani na hususan wakimbizi ni kinyume cha makubaliano na sheria za kimataifa.