Hukumu ya mahakama ya Ulaya dhidi ya vazi la hijabu
Mahakama ya Haki ya Ulaya (ECJ) yenye makao yake huko Luxembourg jana Jumanne ilipasisha marufuku ya vazi la staha la mwanamke wa Kiislamu, hijabu.
Kwa mujibu wa hukumu ya mahakama hiyo, waajiri wa Ulaya wanaweza kuwazuia wafanyakazi wao kuvaa nembo za kidini likiwemo vazi staha la hijabu.
Hii ni hukumu ya kwanza kutolewa na mahakama ya Ulaya kuhusu mjadala wa vazi la staha la mwanamke wa Kiislamu, hijabu katika maeneo ya kazi. Mahakama ya Haki ya Ulaya iliyochunguza mafaili na matukio ya kufutwa kazi wanawake wawili wanaovaa vazi la hijabu katika nchi za Ubelgiji na Ufaransa imetangaza kuwa, ni haki ya kisheria ya kila shirika na kampuni kuwataka wafanyakazi wao kuwa na muonekano usioegamea upande wowote wala kuwa na alama za kidini, na mahakama hiyo imeruhusu mashirika kuzuia alama na nembo za kisiasa, kifalsafa au kidini.
Hukumu hiyo ya mahakama ya Ulaya ya ECJ kwa hakika imetolewa kwa shabaha ya kuzuia vazi la staha la wanawake wa Kiislamu, hijabu wanaofanyakazi katika makampuni na taasisi mbalimbali za Ulaya. Hatua hii si tu kwamba ni ubaguzi wa wazi dhidi ya wanawake wa Kiislamu, bali pia imewapa mamlaka makubwa waajiri kutumia hukumu hiyo kwa ajili ya kuwabana zaidi wafanyakazi wa kike Waislamu na kuwapa hiari ya ama kuvua mavazi yao ya hijabu au kufutwa kazi.
Ubaguzi dhidi ya wanawake Waislamu barani ulaya hauishii katika masuala makhsusi bali unagusa hata masala yao ya kijamii, kisiasa, kiutamaduni na hata kiuchumi na sekta ya ajira. Wimbi kubwa la propaganda chafu za kupiga vita Uislamu na Waislamu (Islamophobia) katika nchi za Magharibi limeisababishia vizingiti vingi na mbinyo mkubwa jamii ya Waislamu barani Ulaya. Kwa mfano tu ripoti iliyotolewa mwaka jana na Kamati ya Wanawake na Usawa ya Bunge la Uingereza ilieleza kuwa, Waislamu wanabaguliwa sana nchini humo katika maeneo ya kazi hususan katika suala la mishahara. Wimbi la chuki na hujuma dhidi ya Waislamu barani Ulaya inafanyika kupitia njia mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuwazulia kesi za aina mbalimbali, kuvunjia heshima matukufu yao ya kidini, propaganda chafu dhidi ya Uislamu na Waislamu na ubaguzi wa kijamii, kiuchumi na kadhalika. Ubaguzi huo sasa unaoekana katika sura ya kukataa kuwaajiri Waislamu au kuwawekea masharti magumu yanayokinzana na imani zao za kidini kama vile kuwazuia wafanyakazi Waislamu wa kike kuvaa vazi la staha la hijabu.
Wakati huo huo wimbi la wakimbizi kueleka katika nchi za Ulaya ambao wengi wao ni Waislamu, limezidisha chuki na propaganda chafu dhidi ya wageni na Waislamu barani humo. Wimbi hilo linaambatana na hujuma kubwa ya kipropaganda ya makundi yenye misimamo mikali ya mrengo wa kulia ambayo yanawalenga hata Waislamu waliozaliwa na kukulia katika nchi za Magharibi.
La kusikitisha zaidi ni kuwa, kwa sasa hakuna mwanga wa matumaini ya kupatikana faraja kwa Waislamu huko katika nchi za Magharibi na hapana shaka kuwa, hukumu ya Mahakaya ya Haki ya Ulaya (ECJ) itachochea zaidi hujuma, mashinikizo na ubaguzi dhidi ya Waislamu katika nchi za bara hilo ambazo zimekuwa zikidai kuwa vinara wa demokrasia na haki za binadamu!