Mwenyekiti wa Kamisheni ya Ulaya: Trump atazusha vita vingine Balkan
https://parstoday.ir/sw/news/world-i26818-mwenyekiti_wa_kamisheni_ya_ulaya_trump_atazusha_vita_vingine_balkan
Mwenyekiti wa Kamisheni ya Ulaya amesema kuwa mienendo na mielekeo ya Rais Donald Trump wa Marekani itasababisha vita vipya katika eneo la Balkan huko Ulaya.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Mar 24, 2017 22:21 UTC
  • Mwenyekiti wa Kamisheni ya Ulaya: Trump atazusha vita vingine Balkan

Mwenyekiti wa Kamisheni ya Ulaya amesema kuwa mienendo na mielekeo ya Rais Donald Trump wa Marekani itasababisha vita vipya katika eneo la Balkan huko Ulaya.

Jean-Claude Juncker ameliambia gazeti la Financial Times la Uingereza kwamba, mitazamo ya Donald Trump kuhusu Umoja wa Ulaya (EU) na sera zake za kuzihamasisha nchi wanachama wa umoja huo kujiondoa kwenye EU zitazusha vita vingine katika eneo la Balkans.

Mwenyekiti wa Kamisheni ya Ulaya amesema kuwa, katika mazungumzo yake na Makamu wa Rais wa Marekani, Mike Pence ameitahadharisha Washington kuhusu mwenendo wa kuzihamasisha nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya kujiondoa katika umoja huo na taathira zake mbaya.   

Hitilafu za EU na Marekani zilionekana waziwazi katika mazungumzo ya Trump na Lansela wa Ujerumani, Angela Merkel

Juncker amesema kuwa, amestaajabishwa na msimamo wa Trump wa kushangilia hatua ya Uingereza ya kujiondoa kwenye Umoja wa Ulaya.

Umoja wa Ulaya na serikali mpya ya Marekani zinahitilafiana katika masuala kadhaa ikiwa ni pamoja na biashara ya kimataifa, gharama za sekta ya ulinzi na mikataba ya mazingira na hali ya hewa.