Apr 07, 2017 07:24 UTC
  • UN yashangazwa na wito wa Trump wa kuwatesa na kuwanyanyasa washukiwa

Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa ameeleza kusikitishwa kwake na wito wa Rais wa Marekani Donald Trump wa kutaka kurejeshwa sheria ya kuwatesa watuhumiwa wa jinai mbalimbali.

Zeid Ra'ad al-Hussein amesema mbinu hiyo ya kuwatesa watuhumiwa ni ya kipuuzi, isiyo na maana na inayokiuka misingi ya haki za binadamu.

Akihutubia wanachuo katika Chuo Kikuu cha Vanderbilt jimboni Tennessee, Zeid Ra'ad al-Hussein, Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa amesisitiza kuwa: "Binafsi nimeshangazwa na namna Trump anavyoshinikiza hadharani kutumiwa mbinu ya mateso, udhalilishaji na unyanyasaji dhidi ya watuhumiwa wa ugaidi, mbinu hizo ni hatari mno kwa mtazamo wa sheria za kimataifa, na zilizopitwa na wakati."  

Sehemu ya mateso kwa washukiwa wa ugaidi

Mapema mwaka huu, maafisa waliostaafu wa jeshi la Marekani wakiwemo majenerali 33 walimwandikia barua Donald Trump wakimtahadharisha kuhusu utekelezaji wa aina mbalimbali za mbinu za kuwatesa watu wanaodhaniwa kuwa na uhusiano na vitendo vya kigaidi. 

Katika kampeni zake za uchaguzi wa rais, Trump alisisitiza kwamba atatumia mbinu kali zaidi za mateso na manyanyaso wakati wa kuwasaili washukiwa wa ugaidi. 

Tags