Apr 12, 2017 14:19 UTC
  • Russia yakosoa misimamo inayokinzana na yenye kutia wasiwasi ya Marekani

Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia ameitaja misimamo ya Marekani katika eneo la Mashariki ya Kati kuwa inayokinzana na yenye kutia wasiwasi.

Sergei Lavrov amesema kuwa msimamo wa Marekani kuhusu uhusiano kati yake na Russia ni wenye kukinzana na kwamba eneo la Mashariki ya Kati linashuhudia mienendo inayotia wasiwasi ya Washington na khususan kuhusu kushambuliwa Syria. Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia ameyasema hayo leo katika mazungumzo na Rex Tillerson Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Marekani aliyeko ziarani mjini Moscow. 

Lavrov ameongeza kuwa, siasa za Moscow zimejengeka juu ya ulazima wa kuheshimiwa sheria za kimataifa. Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia amebainisha kuwa Moscow iko tayari kuanzisha mazungumzo muhimu na ya kiadilifu kulingana na sheria za kimataifa. Lavrov amesisitiza pia kuwa lililo muhimu ni kuwa, mashambulizi ya Marekani dhidi ya Syria yasikaririwe tena na kwamba suala la kushirikiana Moscow na Washington linapaswa kuwekwa wazi. Katika mazungumzo hayo naye Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Marekani Rex Tillerson ametaka kukatwa uhusiano kati ya Moscow na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran; ombi lililokabiliwa na radiamali hasi kutoka kwa viongozi wa Russia.

Rex Tillerson Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Marekani na mwenzake wa Russia, Sergei Lavrov (kulia) huko Moscow

Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia amefanya mazungumzo hayo na mwenzake wa Marekani kufuatia mashambulizi ya kifedhuli yaliyofanywa na Marekani katika ardhi ya Syria. Moscow imechukua msimamo thabiti wa kupinga hatua hiyo ya ikulu ya Marekani (White House) huko Syria na wakati huo huo imelitaka Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuitisha kikao kuchunguza sualal hilo. Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia awali ilisisitiza kwamba Rais wa nchi hiyo Vladimir Putin hatakutana na kufanya mazungumzo na Rex Tillerson Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Marekani. 

Tags