Mar 11, 2016 03:39 UTC
  • Russia yapinga matamshi ya Waziri wa Ulinzi wa Marekani

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia amepinga vikali matamshi yaliyotolewa na Waziri wa Ulinzi wa Marekani dhidi ya Moscow akisema kuwa yanaweka hatarini mchakato wa kurejesha amani nchini Syria.

Maria Zakharova amelaani vikali matamshi yaliyotolewa na Waziri wa Ulinzi wa Marekani, Ashton Carter kuhusu suala la kuiwekea mashinikizo Russia na kusema matamshi ya maafisa wa Marekani dhidi ya Russia hayakubaliki na yanalaaniwa katika mahusiano ya kidiplomasia ya kimataifa.

Mwanzoni mwa mwezi uliopita wa Februari Waziri wa Ulinzi wa Marekani, Ashton Carter alizitaka nchi za Magharibi kushirikiana na kuchukua hatua za kivitendo za kiuchumi na kisiasa dhidi ya kile alichokiita vitisho vya Russia.

Maria Zakharova amesema matamshi kama hayo ya viongozi wa Marekani yanatishia mwenendo wa kusitisha vita nchini Syria wakati Moscow inafanya jitihada za kushirikiana na Washington katika masuala ya Syria. Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia amesisitiza kuwa, mwenendo huo haukubaliki katika mahusiano ya kimataifa.

Marekani na waitifaki wake kama Saudi Arabia, Qatar, Uturuki na Israel zimekuwa zikiyaunga mkono makundi ya kigaidi kama Daesh huko Syria kwa shabaha ya kuiondoa madarakani serikali halali ya nchi hiyo.

Tags