May 05, 2017 13:37 UTC
  • Marekani yakiri kuhusika na shambulizi dhidi ya msikiti nchini Syria

Wizara ya Ulinzi ya Marekani (Pentagon) hatimaye imekiri kuwa ndege za kijeshi za US zilitekeleza shambulizi a anga dhidi ya msikiti mmoja nchini Syria ambapo makumi ya watu waliuawa.

Maafisa wawili wa Pentagon wameiambia kanali ya televisheni ya CCN kuwa, ni kweli Marekani ilitekeleza hujuma hiyo ya anga dhidi ya msikiti mwezi Machi mwaka huu, magharibi mwa mji wa Aleppo (Halab).

Siku moja baada ya shambulizi hilo, Msemaji wa Pentagon, Jeff Davis alikanusha madai kuwa US ililenga msikiti katika hujuma yake hiyo ya anga na kudai kuwa walishambulia ngome ya kundi la kigaidi la al-Qaida.

Mwezi uliopita wa Aprili, shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch lililaani shambulizi hilo la anga la Marekani dhidi ya msikiti na kusisitiza kuwa Washington ilishindwa kuchukua hatua za tahadhari kabla ya kutekeleza shambulizi hilo.

Shughulia za uokoaji baada ya hujuma ya US dhidi ya msikiti Syria

Kadhalika Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kupitia msemaji wa Wizara yake ya Mambo ya Nje, Bahram Qassemi ililaani hujuma hiyo na kusema: "Kushambulia maeneo matukufu na ya kidini kwa lengo lolote lile ni jambo linalolaaniwa na haliwezi kuhalalishika hata kidogo."

Machi 16, raia wasiopungua 49 waliuawa katika shambulio hilo la anga la US lililolenga Msikiti wa Umar Ibn Al-Khaṭṭab uliokuwa umejaa waumini ndani yake karibu na mji wa Halab kaskazini mwa Syria. Watu wengine zaidi ya 100 walijeruhiwa katika shambulio hilo lililofanywa katika kijiji cha al-Jineh kilichopo kilomita 30 magharibi mwa mji wa Halab. 

Tags