May 14, 2017 12:43 UTC
  • Russia: Marekani ni magaidi wa mitandaoni

Makamu wa kwanza wa mkuu wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Baraza Shirikisho la Russia amesema kuwa, kitendo cha wadukuzi wa Marekani cha kudukua mawasiliano ya kompyuta ya nchi mbalimbali duniani, ni ugaidi wa kimitandao.

Shirika la habari la IRNA limemnukuu Frants Klintsevich akisema kuwa, shambulio la dunia nzima la wadukuzi wa mitandao ya mawasiliano ya kompyuta lililofanywa kwa usimamizi na mipango ya Shirika la Usalama wa Taifa la Marekani NSA ni mkubwa sana na ni ugaidi wa mitandao.

Kwa mujibu wa afisa huyo wa ngazi za juu wa Russia, mashambulizi wa wadukuzi hao ni tishio la moja kwa moja kwa maeneo nyeti na muhimu ya jamii ya mwandamu na yameitumbukiza dunia kwenye ugaidi wa mawasiliano ya kompyuta.

Frants Klintsevich, Makamu wa kwanza wa mkuu wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Baraza Shirikisho la Russia

 

Mitandao ya kompyuta wa nchi mbalimbali duniani ikiwemo Russia, imeshambuliwa na wadukuzi wa mawasiliano ya kompyuta tangu siku ya Ijumaa ambao wanatuma virusi vya kompyuta vya kuchafua mitandao hiyo na kufunga uwezo wao wa kutoa taarifa na baadaye kuitaka mitandao hiyo itoe kikomboleo ili wadukuzi hao waiachilie huru.

Edward Snowden, afisa wa zamani wa Shirika la Usalama wa Taifa la Marekani NSA amesema kuwa, shirika hilo ndilo linalohusika na mashambulizi ya mitandao ya kompyuta duniani na hadi hivi sasa limeshashambulia mitandao ya nchi 74 katika kona mbalimbali za dunia. 

Tags