FAO: Idadi ya watu walioathiriwa na njaa itaongezeka
(last modified Mon, 03 Jul 2017 13:01:44 GMT )
Jul 03, 2017 13:01 UTC
  • FAO: Idadi ya watu walioathiriwa na njaa itaongezeka

Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) limesema kuwa, watu milioni 20 wanasumbuliwa na njaa na utapiamlo kote duniani.

Mkurugenzi Mkuu wa FAO, José Graziano da Silva ambaye alikuwa akihutubia mkutano wa siku sita wa jumuiya hiyo katika mji mkuu wa Italia, Roma amesema kuwa, njaa inabidi ikomeshwe kote duniani kufikia mwaka 2030 na kuongeza kuwa, vita na mapigano yanayoongezeka katika nchi mbalimbali ni miongoni mwa sababu za mgogoro wa njaa duniani.

Mkutano wa 40 wa Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) ulioanza tarehe 3 Julai na utaendelea hadi tarehe 8 mwezi huu, utachagua wanachama na mwenyekiti mpya wa baraza la shirika hilo.

Njaa imeathiri nchi nyingi duniani

Mkutano huo ndio kikao muhimu zaidi cha kuchukua maamuzi na hufanyika mara mbili kwa mwaka ukishirikisha marais wa baadhi ya nchi, mawaziri wa kilimo na maafisa wa ngazi mbalimbali wa nchi 194 wanachama wa FAO. 

Mkutano wa mwaka huu unajadili hali ya upatikanaji wa chakula, jinsi ya kusimamia ukame na uhaba wa maji, kilimo cha familia, jinsi ya kupunguza hasara za mazao ya kilimo na kadhalika. 

Tags