Mar 16, 2016 16:39 UTC
  • The Atlantic: Kerry amekuwa akimtaka sana Obama aishambulie Syria

Mtandao wa habari wa The Atlantic wa nchini Marekani umefichua kuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo amekuwa akimtaka mara kadhaa Rais Barack Obama aishambulie Syria kwa makombora.

Kwa mujibu wa mtandao huo, John Kerry amekuwa akimtaka Rais Obama kutekeleza hujuma hiyo kwa kile anachokisema kuwa hiyo ndio njia pekee ya kumlazimisha Rais Bashar al-Assad, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Russia, kukubaliana na matakwa ya Washington.

Aidha mtandao huo umefichua kuwa, kwa kipindi cha mwaka mmoja uliopita waziri huyo wa mambo ya nje wa Marekani amekuwa akiwasilisha pendekezo hilo linalokengeuka haki ya kujitawala Syria. Umeongeza kuwa, kwa mujibu wa Kerry, mashambulizi hayo ya makombora yangetakiwa kufanywa majira ya usiku na katika maeneo husika nchini Syria ili kumuondoa madarakani rais wa nchi hiyo anayeungwa mkono na raia. Hata hivyo Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani John Kerry amedai kuwa mashambulizi hayo si kwa ajili ya kutaka kumuondoa madarakani Rais Bashar al-Assad wa Syria na kwamba ni kwa lengo tu la kumshinikiza rais huyo na nchi waitifaki wake, yaani Iran na Russia kuweza kukaa kwenye meza ya mazungumza.

Kwa mujibu wa mtandao huo wa habari wa The Atlantic, Kerry anaamini kuwa, makombora ya cruise yanaweza kumlazimisha Rais Assad na waungaji wake mkono kuachana na misimamo yao. Ripoti hiyo inaonyesha ni namna gani Marekani na waitifaki wake walivyoshindwa vibaya nchini Syria.

Tags