Marekani yakiri kushindwa kukabiliana na hujuma za kimtandao wakati wa uchaguzi
Wataalamu wa mtandao wa nchini Marekani (Cyber) wamekiri kushindwa vyombo vya upelelezi vya nchi hiyo kulinda usalama wa kimtandao wakati wa uchaguzi.
Edward Felten, mmoja wa wakurugenzi wakuu wa teknelojia nchini Marekani ametoa ripoti ya uchunguzi wake na Taasisi ya Kitaifa na Viwango na Teknolokia nchini Marekani, inayoonyesha kwamba, kuna uwezekano wa kudukuliwa vyombo vya kukusanya matokeo na kupigia kura wakati wa uchaguzi.
Wakati huo huo Anthony Ferrante kiongozi wa zamani wa Idara ya Radiamali ya Kimtandao ameliambia Baraza la Usalama wa Taifa nchini Marekani kwamba, akthari ya raia wa nchi hiyo hawana imani tena na mfumo wa uchaguzi ndani ya taifa hilo.
Matokeo ya utafiti wa taasisi ya Gallup yaliyotolewa hapo kabla yakionyesha kwamba, karibu asilimia 66 ya Wamarekani hawana imani tena na mfumo wa uchaguzi nchini humo. Kwa mara kadhaa Rais Donald Trump amekuwa akisisitiza suala la kuwepo udanganyifu katika uchaguzi wa mwaka 2016 nchini humo.
Kukiri kwa Washington juu ya udanganyifu wa uchaguzi nchini humo kunajiri katika hali ambayo daima taifa hilo limekuwa mstari wa mbele katika kujifanya polisi wa dunia kwa kukosoa chaguzi za mataifa mengine ya dunia.