Aug 01, 2017 02:37 UTC
  • Russia yawapa masaa 72 wanadiplomasia wa Marekani kuondoka nchini humo

Msemaji wa Ikulu ya Rais wa Russia, Kremlin, ametangaza kuwa, wanadiplomasia wa Marekani wamepewa masaa 72 kuwa wamendoka katika ardhi ya nchi hiyo.

Dmitry Peskov amesema kuwa, hatua hiyo ya kuwafukuza wanadiplomasia wa serikali ya Washington imechukuliwa kujibu mwenendo kama huo uliofanywa na Marekani dhidi ya wanadiplomasia wa Russia. 

Peskov amekadhibisha uvumi kwamba Moscow imeghairi uamuzi wa kuwatimua wanadiplomasia wa Marekani katika ardhi ya Russia na kusema kuwa, uamuzi huo umechukuliwa kulingana na misimamo ya Marekani yenyewe. 

Dmitry Peskov

Wakati huo huo afisa mmoja wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani ameeleza kusikitishwa kwake na hatua hiyo ya Russia na kusema kuwa, Washington inachunguza suala hilo. 

Ijumaa iliyopita Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia ilitangaza kuwa, Moscow imeitaarifu serikali ya Washington kwamba, inawajibika kupunguza idadi ya wafanyakazi wa ubalozi wake na ofisi ya ubalozi mdogo wa nchi hiyo nchini Russia na kuwa sawa na idadi ya wafanyakazi wa ofisi za kidiplomasia za Russia nchini Marekani. 

Tags