Aug 02, 2017 08:08 UTC
  • Magaidi washambulia msikiti kwa bomu na kuua makumi, Afghanistan

Habari kutoka Afghanistan zinaarifu kwamba, makumi ya watu wameuawa na wengine wengi kujeruhiwa katika shambulio la kigaidi dhidi ya msikiti mmoja wa Waislamu wa madhehebu ya Shia lililotokea jana jioni mjini Herat, magharibi mwa nchi hiyo.

Duru za hospitali zinasema zaidi ya watu 20 wameuawa katika hujuma hiyo.  Rafeeq Shirzai, msemaji wa Hospitali Kuu ya Herat amesema, maiti 20 zimepelekwa katika hospitali hiyo, huku majeruhi karibu 30 wakiendelea kutibiwa.

Baadhi ya vyombo vya habari nchini humo vimetangaza kuwa, waliouawa katika shambulizi hilo la bomu ni watu 33. 

Polisi ya Afghanistan imesema kuwa, kuna uwezekano idadi ya wahanga wa hujuma hiyo ikaongezeka, kutokana na majeruhi wengi kuwa na hali mbaya.

Moja tya magenge ya kigaidi yanayofanya mashambulizi Afghanistan

Shambulizi la jana mjini Herat ni katika mfululizo wa hujuma nyingi zilizoitikisa Afghanistan katika kipindi cha miezi ya hivi karibuni.

Takwimu za Wizara ya Afya nchini humo zinasema kuwa, zaidi ya watu 1,700 wameuawa katika wimbi la mashambulizi ya kigaidi ndani ya miezi sita ya kwanza ya mwaka huu.

Makundi ya Taleban na Daesh (ISIS) yamekuwa yakihusika na hujuma hizo ambazo weledi wa mambo wanazitaja kuwa, ni njama ya madola ya Magharibi ya kutaka kuendelea kuwepo askari wao nchini humo.

Tags