Kukataa Poland kuwapokea wahajiri Waislamu
Serikali ya Poland imetangaza msimamo wake mpya kuhusiana na kupinga kuwapokea wahajiri na kusema kuwa, haitawapokea wahajiri kutoka Mashariki ya Kati na Afrika.
Witold Waszczykowski, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Poland amesema katika mahojiano aliyofanyiwa na shirika la habari la RIA-novosti kwamba, nchi yake iko tayari kupokea wahajiri kutoka Ulaya lakini haikubaliani na mpango wa Umoja wa Ulaya na kwamba, haitawapokea wahajiri kutoka Mashariki ya Kati na kaskazini mwa Afrika.
Wimbi la wahajiri kuelekea barani Ulaya limeibuka mvutano mkubwa pia nchini Poland kama ilivyo kwa nchi nyingine za Umoja wa Ulaya. Nchini Poland nako kumeibuka mjadala mkali kuhusiana na uamuzi kwamba, kila nchi mwanachama wa Umoja wa Ulaya inapaswa kupokea idadi kadhaa ya wahajiri hao.
Nchi ya Poland inapinga vikali sera za Umoja wa Ulaya kuhusiana na kadhia ya wahajiri na ni sababu hiyo ndiyo maana imekuwa ikisimama na kupinga mpango wa kuwagawa kwa idadi sawa wahajiri baina ya nchi wanachama wa umoja huo. Katika ukosoaji wake wa hivi karibuni dhidi ya Umoja wa Ulaya, Waziri Mkuu wa Poland, Beata Szydlo ambaye ni mhafidhina alisisitiza kwamba, katu nchi yake haitasalimu amri mbele ya mashinikizo na masharti ya umoja huo na kwamba, kamwe haitafuata siasa za uwendawazimu za viongozi wa Umoja wa Ulaya.
Mwaka 2015 baada ya Umoja wa Ulaya kukabiliwa na wimbi la wahajiri kutoka Syria na nchi nyingine kadhaa zilizotumbukia katika mgogoro katika eneo la Mashariki ya Kati ulipendekeza mpango wa kuwagawa wahajiri laki moja na sitini elfu baina ya nchi wanachama wa umoja huo, kama utatuzi wa muda mfupi ambao ulilenga kukabiliana na mgogoro huo.
Hata hivyo nchi kadhaa ikiwemo Poland, Hungary na Jamhuri ya Czech zilipinga mpango huo. Sababu kuu ya inayotolewa na nchi hizo ya kupinga kuwapokea wahajiri ni tishio la utambulisho wa kitaifa endapo wahajiri hao wataingia na kuishi katika nchi hizo.
Hata hivyo baada ya kupita takribani miaka miwili ya subira na matarajio, Umoja wa Ulaya umetangaza kuwa, endapo nchi hizo zitaendelea kung'ang'ania msimamo wao wa kukataa kupokea mgawo wao wa wahajiri walioko Italia na Ugiriki, zitakabiliwa na adhabu ya umoja huo.
Poland kwa upande wake inadai kwamba, suala la kukubali kuwapokea wahajiri ni miongoni mwa kadhia za mamlaka ya kitaifa na jambo ambalo liko mikononi mwa tawala za nchi Ulaya. Hata hivyo, Umoja wa Ulaya unapinga vikali tafsiri hiyo ya Poland.
Hivi sasa serikali ya mrengo wa kulia ya Poland inaandamwa na mashinikizo ya Umoja wa Ulaya kutokana na kufanya mambo kinyume na kanuni na sheria za umoja huo.
Chama cha mrengo wa kulia cha Sheria na Uadilifu kinachodhibiti wingi wa viti bungeni, kimepasisha sheria nyingi zenye lengo la kuwa na udhibiti wa Idara za Mahakama, hatua ambayo imekabiliwa na tishio la Umoja wa Ulaya la kusimamisha haki ya nchi hiyo ya kupiga kura za utoaji maamuzi katika asasi za umoja huo. Tishio hilo limemfanya Rais Andrzej Duda wa nchi hiyo aupigie kura ya veto muswada wa Bunge la nchi hiyo.
Kwa sasa inaonekana kuwa, serikali ya Poland imelegeza msimamo wake kuhusiana na suala la kukataa kuwapokea wahajiri baada ya kukabiliwa na tishio la Kamisheni ya Umoja wa Ulaya la kuiadhibu serikali ya Warsaw.
Hata hivyo kisingizio kipya kinachotolewa na Poland kwa aina fulani ni hatua ya kucheza na maneno na mwenendo wa kibaguzi dhidi ya Waislamu baada ya kusema kwamba, haiko tayari kupokea wahajiri Waislamu kutoka Mashariki ya Kati. Hii ni katika hali ambayo, wahajiri amboa filihali wako Ugiriki na Italia wakisubiri kuainishiwa hatima yao, wote wanatoka katika eneo la Mashariki ya Kati na aghalabu yao ni Waislamu.