UN yaikosoa Marekani kwa kuwazuilia wahajiri na wanaotafuta hifadhi
https://parstoday.ir/sw/news/world-i33160-un_yaikosoa_marekani_kwa_kuwazuilia_wahajiri_na_wanaotafuta_hifadhi
Wataalamu wa masuala ya haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa wamekosoa kitendo cha Marekani kuendelea kuwazuilia wahamiaji na raia wa kigeni wanaotafuta hifadhi nchini humo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Aug 14, 2017 23:26 UTC
  • UN yaikosoa Marekani kwa kuwazuilia wahajiri na wanaotafuta hifadhi

Wataalamu wa masuala ya haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa wamekosoa kitendo cha Marekani kuendelea kuwazuilia wahamiaji na raia wa kigeni wanaotafuta hifadhi nchini humo.

Wataalamu hao wa UN wameeleza wasi wasi wao kuhusu kuendelea kuzuiliwa kwa vipindi virefu wahamiaji na watu waliokwenda kutafuta hifadhi nchini humo wakisisitiza kuwa, haki zao wahajiri hao zimekiukwa.

Ripoti ya wataalamu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa imebainisha kuwa, miongoni mwa changamoto wanazopitia wahajiri hao ni pamoja na kuzuiliwa kwa muda mrefu kabla ya kufikishwa mahakamani, kutotafutiwa mawakili wa katika kesi zinazowakabili, ubaguzi na kupatiwa hukumu zisizo za kiadilifu.

Kadhalika wataalamu hao wa UN wamekosoa vikali hatua ya mahakama kutoa hukumu kwa watoto wadogo sawa na hukumu inazotoa kwa watu wazima.

Rais Trump wa Marekani

Mwezi Machi mwaka huu, Rais Donald Trump wa Marekani alipasisha agizo jipya la kibaguzi dhidi ya wahajiri kutoka nchi sita zenye idadi kubwa ya Waislamu ambazo ni Sudan, Somalia, Syria, Iran, Libya na Yemen, ambapo aliiondoa Iraq, iliyokuwa katika orodha ya awali ya nchi saba za Kiislamu ambazo raia na wakimbizi wake hawataruhusiwa kuingia nchini Marekani.

Kamisheni ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa ilikosoa vikali dikrii hiyo na kusema kuwa, amri hiyo ya Trump ya kuzuia raia wa nchi sita za Kiislamu kuingia nchini Marekani na hususan wakimbizi ni kinyume cha makubaliano na sheria za kimataifa, mbali na kuwabagua watu kwa misingi ya dini na imani zao za kiroho.